Watumishi wa Umma mkoani Songwe watakiwa kuiga utendaji kazi wa Rais Magufuli
‘’Ukishaajiriwa serikalini katika ngazi yoyote ya uongozi ujue kuwa wewe ni mwakilishi wa Rais wa nchi yetu katika eneo lako”ni maneno ya Katibu Tawala wa mkoa wa Songwe Ndg.David Kafulila kwa watumishi wa mkoa huo.
Kiongozi huyo aliyasema hayo alipozungumza na watumishi wa umma wa Kata za Itumba na Isongole kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje akiwa katika mfululizo wa ziara zinazomkutanisha na watumishi anaowaongoza mkoani humo.
Alisema kuwa,utendaji kazi wa watumishi wa umma ulenge kuwapunguzia kero wananchi badala ya kusubiri zitatuliwe na viongozi wa ngazi za juu huku wakiwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Ameongeza kuwa kama wananchi wanavyopata tumaini na faraja wanapokutana na Mhe.Rais Magufuli hali hiyo iendelezwe hata kwa vingozi wa ngazi za chini ambazo zinatekeleza maagizo ya serikali iliyopo madarakani.
Pamoja na mambo mengine Ndg.Kafulila aliwataka watumishi wa umma kutojiingiza kwenye migogoro ya kisiasa hususani inapotokea kati ya mwajiri wao na viongozi,akiwataka kuwa chanzo cha utatuzi wa migogoro hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kikao hicho kiongozi huyo aliyeteuliwa kushika wadhifa huo kwenye mkoa mchanga hapa nchini amekuwa akekerwa na utendaji kazi wa mazoea unaochelewesha huduma kwa wananchi.
Kwa upande wao watumishi hao walimweleza namna utendaji kazi wao unavyokwama na kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa ukiwemo upungufu wa watumishi wenyewe pamoja na uhaba wa vitendea kazi.
Gloria Kang’oma Afisa Elimu Sekondari alisema kuwa uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi limekuwa tatizo kukiwa na mahitaji ya walimu 139 waliopo ni 83 wakipungua walimu 56 hali aliyosema inakwamisha kuzalisha wanasayansi wa badaye.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa