Halmashauri ya Wilaya ya Ileje inaendelea na zoezi la utambuzi wa mifugo sambamba na utoaji wa chanjo kwa ng’ombe kwa bei ya ruzuku kutoka Serikali Kuu, ambapo mfugaji atachangia kiasi cha Sh. 500 kwa kila mfugo, huku gharama nyingine ikilipiwa na Serikali. Zoezi hili lina lengo la kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng’ombe pamoja na kuimarisha afya na ubora wa mifugo.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mratibu wa utambuzi na chanjo ya mifugo Wilaya ya Ileje, Dkt. Alfred Richard Kasindi, ametoa wito kwa wafugaji wote kujitokeza kwa wingi kupeleka mifugo yao ili iweze kuchanjwa pamoja na kuwekewa hereni za utambuzi (ear tag). Aidha, Dkt. Alfred amewatoa hofu wafugaji kuwa chanjo hizo ni salama kwa mifugo yao na hazina madhara yoyote. Amesema hatua hiyo ni sehemu ya ajenda ya Serikali katika kuboresha na kuinua sekta ya mifugo ili kuhakikisha wafugaji wanapata mazao bora na yenye tija.
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Ileje inatarajia kuchanja na kuweka hereni kwa jumla ya ng’ombe 45,000 katika maeneo yote ya wilaya hiyo.
Wafugaji wote wanahamasishwa kuchangamkia fursa hii adimu yenye lengo la kuwainua, kuhakikisha mifugo inazaliana kwa wingi, kuepusha hasara zitokanazo na matibabu endapo mifugo haitopata chanjo, pamoja na kuzuia vifo vya wanyama.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa