Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Bi. Nuru Waziri Kindamba, ametoa rai kwa Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji pamoja na Watendaji wa Vijiji kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na misingi ya utawala bora katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi.
Bi. Kindamba alitoa wito huo wakati wa hafla ya ufunguzi wa semina ya mafunzo kwa viongozi hao, iliyofanyika hivi karibuni wilayani Ileje, yenye lengo la kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali ya kiuongozi na kiutendaji.
Semina hiyo, inayoratibiwa na kuendeshwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo, inalenga kuimarisha uongozi na utawala bora, uibuaji, upangaji na usimamizi wa miradi shirikishi, usimamizi wa ardhi na udhibiti wa uendelezaji wa miji, pamoja na uendeshaji sahihi wa vikao na mikutano ngazi ya kijiji na kata. Vilevile, washiriki wanapatiwa mafunzo juu ya usimamizi wa manunuzi kwa mujibu wa sheria na taratibu za mamlaka za Serikali za Mitaa.
Akizungumza katika hotuba yake, Bi. Kindamba alisema viongozi wa ngazi za vijiji na vitongoji ndio kiungo muhimu kati ya wananchi na serikali, hivyo maamuzi na maelekezo yao yanapaswa kusimama kwenye msingi wa haki, uwajibikaji na uadilifu.
“Ni wajibu wa kila kiongozi wa ngazi hizi kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki, na huduma hizo lazima zitekelezwe kwa kuzingatia sheria, kanuni pamoja na misingi ya utawala bora. Hii ndio njia pekee ya kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao,” alisisitiza.
Aidha, DED Kindamba alihimiza washiriki wa semina hiyo kuipa kipaumbele ajenda ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa uwazi na ufanisi, akiwataka kushirikiana kwa karibu ili kudhibiti changamoto ya ukwepaji wa mapato.
“Mapato ndio nguzo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo kila mmoja wenu lazima awe sehemu ya kuhakikisha kila shilingi inayokusanywa inaleta matokeo chanya kwa wananchi. Tukidhibiti mianya ya ukwepaji wa mapato, tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika maendeleo ya Wilaya ya Ileje,” ameongeza Bi. Kindamba.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa semina hiyo wamepongeza hatua ya Halmashauri kuandaa mafunzo hayo, wakieleza kuwa yatawasaidia kuongeza maarifa na uelewa juu ya sheria na taratibu za Serikali za Mitaa, jambo litakalowawezesha kusimamia vyema shughuli za kiserikali katika maeneo yao.
Semina hiyo inatarajiwa kujikita zaidi katika mafunzo ya vitendo na mijadala shirikishi, ili kuhakikisha viongozi wanakuwa na uelewa mpana kuhusu namna bora ya kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi na kuchochea maendeleo endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
![]() |
![]() |
![]() |
![]() |
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa