Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuilinda na kuitunza amani ambayo ni miongoni mwa Tunu muhimu za Taifa la Tanzania.
Akizungumza mapema leo Oktoba 16, 2025 kupitia kipindi maalumu cha Radio Jamii Ileje FM, 105.3, ambapo aliambatana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ileje, Mrakibu Mwandamizi Wa Polisi (SSP) Kennedy J. Msukwa kwa pamoja wametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kwa Amani, Utulivu na Umoja.
Aidha, DC Mgomi amewahakikishia wananchi kuwa Wilaya ya Ileje ipo salama, huku akibainisha kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha zoezi la Uchaguzi linafanyika kwa utulivu , huku hali ya amani ikiendelea kudumu na hata baada ya uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu, kwa kuhabarishana na kusambaza taarifa zenye manufaa kwa jamii, na kuepuka kusambaza taarifa za uongo, chuki au zinazoweza kuvunja Amani na Mshikamano wa Wananchi. Huku akisisitiza pia umuhimu wa vyombo vya habari kuwa daraja la kuhubiri amani, upendo na utulivu katika jamii hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ileje SSP. Kennedy J. Msukwa amewataka wananchi kushirikiana bega kwa bega na Jeshi la Polisi katika kulinda amani, pamoja na kukemea matendo yanayoweza kusababisha vurugu au uvunjifu wa amani. Amewataka wananchi kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu , sambamba na kuheshimu mawazo na mitazamo ya wengine licha ya tofauti au itikadi za kichama zilizopo baina yao.
Kwa kuhitimisha, Mheshimiwa Farida Mgomi pamoja na Kamanda wa Polisi wa Wilaya wamewasihi wananchi wa Ileje na Tanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi, huku wakisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa Taifa.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa