Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, ametoa shukurani kwa wadau wa maendeleo kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha ustawi wa Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kijamii, hususan katika sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Itete, ujenzi unaofadhiliwa na wadau wa maendeleo wakiongozwa na Dkt. Innocent Mhagama, mzawa wa kijiji hicho, kwa kushirikiana na Shirika la Antonia Development Fund kutoka Uholanzi, Mheshimiwa Mgomi alisema hatua hiyo ni ya kupongezwa kwani inaleta tija kwa wananchi wa Ileje.
Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo aliwapongeza wadau hao kwa kujitolea kuwekeza katika sekta ya afya, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma bora kwa wananchi wa Kijiji cha Itete na maeneo jirani.
Vilevile, Mheshimiwa Mgomi amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Itete kwa kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha jengo la zahanati hiyo linasimama, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni kielelezo cha umoja na uzalendo katika kuunga mkono juhudi za serikali.
Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kuboresha sekta ya afya kwa ushirikiano yakinifu na wadau wa maendeleo, ili kufanikisha adhima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amedhamiria kuimarisha sekta ya afya kama msingi wa maendeleo endelevu ya taifa kwa ujumla.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa