Wanafunzi wa Shule za Sekondari wilayani Ileje wamepata elimu ya uzalendo huku wakitakiwa kutafsiri kwa vitendo elimu hiyo na kulifanya Taifa kuwa na raia wenye uzalendo wa kweli.
Zoezi hilo,limefanyika ukiwa mfululizo wa mafunzo hayo kwa shule zenye Kidato cha Tano na Sita likiratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe kupitia Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Masuala ya Elimu Ndg.Juma Kaponda kwa ushirikiano na mwandishi wa kitabu cha Uzalendo kijana Joel Nauka.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanafunzi wa shule za Kafule na Ileje Ndg.Kaponda aliupongeza uongozi wa Shule ya sekondari Ileje kwa jinsi walivyotumia vema pesa za ujenzi wa vyumba vya madarasa,mabweni na vyoo akisema huo ndio uzalendo unaotakiwa katika Taifa hili.
Naye,mtaalam wa mada hiyo Ndg.Joel Nauka aliwaeleza wanafunzi juu ya sifa anazotakiwa kuwa nazo mzalendo wa kweli kuwa pamoja ni kuichukia rushwa,kusaidia watu wengine,kuthamini utamaduni wake pamoja na kuwa tayari kulifia taifa la Tanzania.
Alisema kuwa nyumbani halisi kwa kila Mtanzania ni Tanzania na si katika taifa jingine,umoja upendo na mshikamano havina budi kupandwa mioyoni mwa vijana ili kuepuka madhara yatokanayo na kukosekana kwa uzalendo kama ilivyo kwa mataifa mengine.
Baadhi ya wanafunzi walisema kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa muda mwafaka kwani kuna vijana wengi wamekosa misingi ya uzalendo.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa