Katika kuhakikisha Mkoa wa Songwe unawaletea wananchi maendeleo Mkuu wa Mkoa huo Bigedia Jenerali Nicodemas Mwangela ameridhishwa na kasi ya utendaji inayooneshwa na baadhi ya viongozi wakiwemo Wahe.Wabunge tangu kuchaguliwa kwao mwishoni mwezi Oktoba 2020.
Akizungumza katika kikao cha ufunguzi wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mapema leo Ijumaa 11/12/2020 katika ukumbi wa Sekondari ya Itumba alisema kuwa anaridhishwa na kasi ya Wahe.Wabunge katika kuwahudumia wananchi hata kabla ya kuapishwa kwao.
Mwangela aliongeza kuwa juhudi za Mhe.Rais Magufuli katika kuwatumikia watanzania hazina budi kuungwa mkono na Wahe.Madiwani kwa kushirikiana na watalaam wa maeneo yao wakiwa wabunifu kulingana na maeneo yao pamoja na rasilimali zilizopo.
Pamoja na mambo mengine RC huyo aliwataka wateule hao kusimamia mapato na kulinda hadhi ya serikali kwa kujiepusha na mambo ya aibu ambayo huwagharimu wakati wa uchaguzi.
Aidha,aliwataka viongozi kushikamana katika kuandaa vyumba vya madarasa pamoja na madawati ili kuwawezesha wanafunzi waliochaguliwa kuingia Kidato cha Kwanza 2021 wanafanya hivyo ukiwa ni utekelezaji wa maagizo ya serikali pamoja na kuwawezesha watoto hao kupata elimu ambayo ni moja ya haki zao.
Joseph Mkude Mkuu wa Wilaya hiyo akizungumza katika kikao hicho aliwataka Wahe.Madiwani kuachana na fikra za Mchaguzi Mkuu uliopita badala yake wajielekeze katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya 2020-2025.
Mohamed Mwala Diwani wa Kata ya Itumba aliwaomba madiwani wenzake kuzungumzia maslahi ya Halmashauri badala ya wilaya ya kata,kanda na tarafa.
Zoezi la kuapishwa kwa Wahe.Madiwani mkoani Songwe na hapa nchini kwa ujumla limekuwa likiendelea ili kuhalalisha nafasi hizo za uongozi zilizopatikana kupitia sanduku la kura.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa