Hayo yameelezwa wakati wa kukabidhi barabara kwa kampuni ya ARI kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mjini Itumba na kwenye eneo la mradi katika Kijiji cha Kapeta katika Kata ya Ikinga wilayani humo.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi alimtaka Mkandarasi wa Mradi huo kuhakikisha anafanya kazi kulingana na mkataba huku akizingatia ubora pamoja na muda uliopangwa kwakuwa fedha zipo kwa mujibu wa TARURA.
Aidha DC Mgomi ameongeza kuwa serikali chini ya Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kwa dhati kuhakikisha inatekeleza Ilani ya Uchaguzi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa barabara hiyo ambayo inalenga kuibua na kuimarisha mgodi pamoja na kiwanda cha makaa ya mawe cha kiwira kilichopo Ileje.
Mhe.Ubatizo Songa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo alieleza kufurahishwa kwake na hatua hiyo akisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaongeza kasi ya uzalishaji katika mgodi wa kiwira hivyo kufungua fursa mbalimbali kwa vijana, wanawake na watanzania kwa ujumla hivyo kuongeza mapato ya ndani.
Mhandisi Benjamini Magese kutoka TARURA makao makuu alisema kuwa fedha hizo zimetokana na tozo hivyo mkandarasi ahakikishe anatoa ajira kwa wakazi wa eneo la mradi hali itakayoleta mahusiano pamoja na usalama wa vifaa kwakuwa jamii hiyo itakuwa sehemu ya mradi.
Wakazi wa eneo hilo waliokutwa wakichapa kazi kwenye kiwanda hicho wakiwa wameanza hivi karibuni wamepongeza serikali kwa hatua hiyo huku wakieleza matarajio yao juu ya ujenzi wa barabara hiyo na uzalishaji wa makaa ya mawe utakavyowaongezea kipato.
Ujenzi huu ukitarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja tayari TARURA walishalima barabara inayotumika kutoka Landani yanapochimbwa makaa ya mawe sasa hadi Kapeta mgodini (maarufu kama STAMICO) yanapochakatwa kimadaraja na kupimwa uzito na kuacha kuzunguka Kyela hali inayotarajiwa pia kumrahisishia kazi mkandarasi wa sasa.
“Awali tulipokuwa tukitumia barabara ya kuzunguka kupitia Wilaya ya Kyela tulisafiri km 76 kwenda na kurudi trip zikiwa tatu tu kwa gari moja sasa kwenda na kurudi ni km 10 tu na sawa tripu 12 za gari moja kwa siku” alisisitiza Mhandisi Peter Maha meneja wa Mgodi wa Makaa ya mawe wa Kiwira.
Ikumbukwe kuwa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira pamoja na kiwanda cha Kiwira kwa muda mrefu haukutangazwa kama upo Ileje lakini kwa umoja wa viongozi wa kisiasa na serikali ngazi ya wilaya ya Ileje pamoja na Mkoa wa Songwe walipaza sauti na hatimaye kuhakikisha kuwa utajiri huu wa asili kusomeka upo Ileje Songwe na si vinginevyo.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa