Akizungumza mara baada yakuapishwa kwake Mhe Suluhu amewataka Watanzania kusahau tofauti zilizopita na kuwa wamoja katika kipindi hiki cha maombolezo ya kuondokewa na mmoja wa mashujaa wa Taifa hili aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli.
Rais huyu anayeandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza katika taifa hili na Afrika ya Mashariki kushika wadhifa wa juu kabisa kwa kuchukua nafasi ya urais baada ya kifo cha Mkuu wake ameonesha ukomavu wa uongozi katika hotuba yake fupi.
Baadhi ya mambo ya kuvutia katika hotuba yake ni pamoja na kushukuru makundi mbalimbali ya kijamii vikiwemo vyama vya kisiasa kwa jinsi vilivyoonesha kushitushwa na kifo cha Rais Magufuli aliyeingia madarakani mnamo mwaka 2015 kwa njia ya sanduku la kura na kushinda tena kwa mara ya pili mwishoni mwa mwaka 2020.
Hotuba yake hiyo fupi imembatana na ratiba nzima ya namna mwili wa marehemu Magufuli utakavyoagwa kuanzia Jumapili 21/3/2021 kule Dar es Salaam hadi siku ya mazishi huko Chato kwenye nyumba yake ya milele.
Hata hivyo mijadala ya msiba na kuapishwa bado haishi vinywani mwa Watanzania juu ya nani atachukua mikoba ya Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassani ili kujua kikosi kazi kitakuwaje kwa miaka hii kabla ya 2025.
Ikumbukwe kuwa Mhe.Samia Suluhu anakuwa Rais wa sita ikiwa ni Awamu ya Tano iliyoanza 2015 akiwa ametanguliwa na wenzake watano ambao watatu kati yao wameshatangulia mbele ya haki.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa