Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Zainab A. Katimba ameyafungua rasmi mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) kwa mwaka 2025 yanayofanyika jijini Tanga.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Mhe. Katimba ametoa rai kwa washiriki wa mashindano hayo kutumia fursa ya michezo kuimarisha mahusiano mazuri baina yao pamoja na kuzitangaza Halmashauri zao kupitia ushiriki wa mashindano mbalimbali. Aidha, amewataka watumishi wote kutumia michezo kama njia ya kuimarisha afya, kuongeza ukakamavu, bidii kazini na kuendeleza uzalendo sambamba na mahusiano bora kwa wananchi.
Vilevile, amewaagiza Wakurugenzi na Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha mashindano haya yanapewa kipaumbele kwa kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu, kwani ni sehemu muhimu ya kujenga mshikamano na mshikamanio wa kitaifa.
Aidha, akirejea kauli mbiu ya mashindano haya isemayo “Jitokeze Kupiga Kura kwa Maendeleo ya Michezo”, Naibu Waziri amewataka watumishi kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi kwa kuwahamasisha kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ili kupata viongozi bora
Mashindano haya ya SHIMISEMITA yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 29 Agosti 2025, ambapo jumla ya Halmashauri 150 zinashiriki katika michezo mbalimbali. Mashindano haya makubwa yanalenga kudumisha mshikamano, mahusiano na mshikamanio miongoni mwa watumishi wa Serikali za Mitaa nchini Tanzania.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa