Jeshi la Magereza Wilaya ya Ileje limeadhimisha kilele cha Wiki ya Magereza kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje iliyopo Itumba na kugawa zawadi kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya kina mama na watoto. Hatua hiyo imeonesha mshikamano wa dhati kati ya Jeshi hilo na wananchi wa Wilaya ya Ileje.
Maadhimisho hayo yamefanyika mapema leo,26 Agosti 2025, ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 64 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza nchini Tanzania. Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Ileje Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP). Abdi Fadhili Mahetha amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuonesha kuwa Jeshi la Magereza, mbali na jukumu lake la kudhibiti na kurekebisha wafungwa, pia lina wajibu wa kushirikiana na jamii katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi Pamoja na kuimarisha mahusiano bora baina ya jeshi hilo na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ileje, Dkt. Lilian Soteri, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya, amelipongeza Jeshi la Magereza wilayani hapa kwa mchango huo akibainisha kuwa hatua hiyo inadhihirisha mshirikiano wa karibu kati ya sekta ya afya na vyombo vya ulinzi.
“Nawashukuru sana Jeshi la Magereza kwa kutuunga mkono kupitia usafi na zawadi kwa wagonjwa. Hii ni ishara ya mshirikiano wa dhati na sisi tunawaahidi kuendeleza mshirikiano huu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya,” alisema Dkt. Soteri.
Mbali na kufanya usafi na kugawa zawadi, Jeshi la Magereza limeahidi kuendeleza utamaduni wa kushiriki katika shughuli za kijamii kila mwaka ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa miaka 64 sasa, Jeshi la Magereza limekuwa chachu ya urekebishaji wa wafungwa kupitia elimu, mafunzo ya ufundi stadi, kilimo na shughuli za uzalishaji mali zinazowawezesha kurejea katika jamii wakiwa na stadi za maisha. Aidha maadhimisho yam waka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Ushirikiano wa Jeshi la Magereza na Jamii kwa Urekebishaji wenye Tija.” ambayo inalenga kusisitiza umuhimu wa mshirikiano kati ya Jeshi la Magereza na wananchi kama nyenzo muhimu ya kujenga Taifa lenye mshikamano, usalama na maendeleo endelevu.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa