Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, ametoa wito kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Ileje na Mkoa wa Songwe kwa ujumla kuchangamkia fursa ya uwekezaji wa vituo vya mafuta katika Wilaya ya Ileje ili kuboresha huduma na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hiyo ambayo inaendelea kufunguka kwa kasi.
Mheshimiwa Mgomi alitoa rai hiyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyabiashara la Wilaya ya Ileje kilichofuatiwa na semina maalum kutoka kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). Semina hiyo ililenga kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi na kueleza taratibu mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya nishati, kwa lengo la kuwahamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo katika eneo hilo.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kusimamia na kutekeleza ajenda ya matumizi ya nishati safi, ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi ikiwemo kupunguza gharama, kuimarisha afya na kutunza mazingira.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mgomi aliwahakikishia wafanyabiashara kuwa serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano wa karibu na kuwaunga mkono katika uwekezaji wa vituo vya mafuta, ili kuhakikisha Wilaya ya Ileje inaendelea kufunguka kiuchumi na kufikia maendeleo endelevu.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa