“Msiwaingize raia wa kigeni katika maboresho ya Daftari la Wapiga Kura”DED wa Ileje awataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Katika kuhakikisha Watanzania wanashiriki vema kwenye Uchaguzi Mkuu ujao Afisa Mwandikishaji wa wa Jimbo la Uchaguzi la Ileje Ndg.Haji Mnasi aliwataka wakazi wa Halmashauri hiyo kulinda zoezi hilo kutoingiliwa na raia wa nchi jirani.
Mnasi alitoa rai hiyo wakati wa kufungua mafunzo ya siku mbili kwa washiriki 38 watakaohusika na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Jimbo hilo yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Sekondari ya Itumba.
“Watendaji wa Kata,vijiji na wananchi wengine tuhakikishe kila mmoja anahusika kulinda usalama wa zoezi hili huku tukijua kuwa tupo mpakani mwa nchi mbili za Zambia na Malawi”aliongeza kiongozi huyo.
Aliongeza kuwa umakini katika zoezi hili utaepusha baadhi ya raia hao wanaoweza kutaka kunufaika na vitambulisho vya mpiga kura ambavyo licha ya uchaguzi vimekuwa na matumizi mengine.
Wilaya ya Ileje ni moja ya wilaya zilizo mpakani ambazo wakazi wake wamekuwa na mahusiano ya kihistoria na nchi jirani za Malawi na Zambia.
Uchaguzi Mkuu hapo nchini unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu ambapo wakati wa maboresho ya daftari hili kila mdau ametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya Covid-19.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa