Wakati sauti za mashirika mbalimbali na vyombo vya habari zikipazwa kutetea haki za watoto kote duniani Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mkoani Songwe amewataka wazazi kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu ambayo ni moja ya haki zao za msingi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Joseph Mkude wakati akitoa baiskeli za tairi tatu kwa watoto wenye uhitaji maalamu (ulemavu wa viungo), Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wenye ulemavu hawafichwi majumbani kwani kwa kufanya hivyo ni kuendeleza vitendo vya unyanyasaji katika jamii.
“Watoto wa aina hiyo hawana budi kuendelezwa kielimu kwani wana vipaji mbalimbali ambavyo vikiendelezwa vitaleta manufaa si kwa familia zao bali hata kwa taifa zima” alisema Mteule huyo wa Rais.
Vifaa hivyo vilivyotolewa kupitia shirika lisilo la Kiserikali la IRADO lililopo Wilayani hapa,viligawiwa kwa baadhi wazazi nawalezi wa watoto toka kata za Mbebe, Isongole, Chitete na Itale ikiwa ni sehemu ya baskeli 15 zilizotolewa siku hiyo.
Akielezea hali ya vitendo vya unyanyasaji Wilayani humo Mkuu wa Wilaya alisema kuwa hakuna matukio ya unyanyasaji kwa watoto wenye ulemavu.
Afisa Elimu - Elimu Maalum (W) Mwalimu Bashiri Msegeya akielezea tukio la kutolewa kwa baiskeli hizo alisema kuwa hiyo ni hatua kubwa katika ukombozi kwa mtoto mwenye ulemavu.
Msegeya aliongeza kuwa Wilaya ya Ileje ina watoto 248 walio shuleni na watoto nane waliweza kujiunga na Elimu ya Sekondari hapo mwaka jana na wamekuwa wakiendelea na masomo.
Hivi karibuni Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2018 Ndugu Charles Kabeho alipongeza juhudi zinazofanywa na Wilaya ya Ileje kwa kutenga shule ya Msingi Ilulu kuwa kituo maalum cha kuhudumia walemavu.
Uchunguzi umebaini kuwepo kwa mahusiano mazuri ya kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa binadamu kati ya Wilaya za Ileje-Tanzania na Chitipa-Malawi ambapo kwenye vikao vya Kiidara vya ujirani mwema wamekuwa wakijadili na kuweka mikakati ya kuwalinda walemavu wa ngozi(albino)na kuzuia biashara ya usafirishaji wa binadamu.s
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa