CHAPENI KAZI MSIOGOPE USHIRIKINA-RC GALAWA
Na:Daniel Mwambene,Ileje
Watumishi wa Umma mkoani Songwe wametakiwa kujikita katika uchapaji kazi badala ya kuhofia kufanyiwa vitendo vya kishirikina katika maeneo yao ya kazi.
Wito huo,ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Mh.Chiku Galawa alipokuwa akizungumza na watumishi wa Idara ya Elimu wilayani Ileje kwenye ukumbi wa Mwala mjini Itumba akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Akijibu kero na vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha taaluma na kupelekea mkoa huo kufanya vibaya katika Mtihani wa Taifa Darasa la Saba 2016 kwa kuwa wa mwisho kitaifa Mh.Galawa alisema kuwa watalaam wa elimu hawana budi kuondokana na hofu ya kufanyiwa vitendo hivyo ambavyo alisema kuwa vinajengwa na dhana ya kufikirika.
Alisema kuwa dhana hiyo ikishakaa akilini huweza kuvuruga uwezo wa utendaji kazi wa mtu huku kila wakati akiwaza kama vile anafanyiwa vitendo hivyo na binadamu wenzake matokeo yake ni kuleta mahusiano mabaya na kutoaminiana kati yao na jamii inayowazunguka au baina ya watumishi.
Aliongeza kuwa,watumishi wamepelekwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Songwe kwa lengo la kuondoa na kupunguza imani kama hizo zinazokwamisha maendeleo.
Mh.Galawa alionesha masikitiko yake kwa watumishi hao jinsi walivyokuwa wakielezea baadhi ya matukio wanayoamini kuwa ni ya kishirikina wakihimiza kuwa yanachangia katika kukwamisha taaluma.
Awali baadhi ya walimu walimweza Mkuu huyo wa Mkoa kuwa ushirikina katika wilaya ya Ileje kwa baadhi ya maeneo kimekuwa chanzo kikuu cha kushuka kwa kiwango cha elimu kwa kuwa walimu wengi wamekuwa wakiogopa kufanya kazi katika maeneo hayo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka watumishi hao kusimama katika imani zao za dini ambazo zinaamini Ukuu wa Mungu kuliko miungu wengine wakiwemo washirikina.
Baadhi ya walimu waliochangia katika kikao hicho walimpongeza Mh.Galawa kwa jinsi anavyofanya kazi ili kuujengea misingi imara mkoa huo mpya wenye umri zaidi ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake ukimegwa toka mkoa wa Mbeya.
Mwalimu Robert Simbeye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Wilayani Ileje alipongeza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa licha ya kupigania maendeleo ya mkoa pia ni ‘mama wa watu’ kwa jinsi anavyosikiliza na kutoa utatatuzi wa shida mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine kiongozi huyo aliwataka watumishi wote kuwa wabunifu katika kuyakbiri mazingira yao ya kazi na kuhakikisha kuwa wanakuwa chachu ya maendeleo ya wananchi.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa