Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Bi Nuru Waziri Kindamba ameongoza kikao cha Menejimenti ya Halmashauri (CMT) kilichoshirikisha pia Watendaji wa Kata zote za Halmashauri hiyo.
Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Halmashauri, ili kuhakikisha kuwa malengo ya makusanyo yanafikiwa kwa wakati na kwa ufanisi.
Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ilifanikiwa kukusanya jumla ya shilingi 2,591,418,267.39, sawa na asilimia 111.15 ya makisio ya mapato ya ndani. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 3,311,221,000.00 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato vilivyopo ndani ya Wilaya.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi Kindamba amewataka Watendaji wa Kata kushirikiana kwa karibu na viongozi wa vijiji na vitongoji ili kusimamia vyanzo vya mapato vilivyopo katika maeneo yao. Aidha, amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika kuongeza mapato na kudhibiti upotevu wa fedha za umma.
Bi Kindamba pia amewataka Watendaji wa Kata kuwa wabunifu katika kuibua vyanzo vipya vya mapato, ili kuongeza mapato na kuhakikisha malengo yaliyowekwa kwa mwaka huu wa fedha yanatimizwa kwa kiwango cha kuridhisha.
Watendaji wa Kata kwa upande wao wameahidi kuimarisha juhudi katika ukusanyaji wa mapato na kushirikiana kikamilifu na menejimenti ya Halmashauri kuhakikisha maendeleo ya wananchi wa Ileje yanapatikana kupitia mapato hayo.
![]() |
![]() |
![]() |
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa