Machifu Ileje waungana na serikali kulinda mazingira.
Ikiwa ni miezi michache imepita tangu Dunia kusherehekea siku ya mazingira ,Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA) wilayani Ileje mkoa wa Songwe umeunga juhudi zinazofanywa na serikali katika kuhifadhi mazingira.
Kauli hiyo ilitolewa hivi katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kilichokuwa kikijadili masuala kadhaa yakiwemo ya amani ndani ya wilaya na taifa kwa ujumla.
Akisoma taarifa hiyo Katibu wa MUJATA wilaya ya Ileje Ndugu Kayolo Msongole alisema kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali katika kampeni ya ulinzi wa miti ya asili pamoja na upandaji miti inayolenga kuliepusha taifa dhidi jangwa.
Alisema kuwa, baadhi ya maeneo machifu wamekuwa walinzi wakubwa wa mazingira na jamii imekuwa ikiwatii lakini baadhi ya maeneo kuna hali ya kudharau maagizo ya aina hiyo yanapotolewa na viongozi hao wa mila.
Maisha Silwimba mjumbe toka Kata ya Chitete alitolea mfano wa maeneo yanayotunzwa kimila yaliyopo katika vijiji vya Mlale na Msia ambayo yanaonesha taswira halisi ya kazi ya machifu ambao alisema serikali isiwatenge katika masuala kama hayo.
Naye Mchungaji Kiongozi Pamesa Mwantemanie wa KKKT Usharika wa Ileje alisema kuwa viongozi wa mila hawana budi kujijengea heshima kwa jamii kwa mienendo yao ili kuwa na sauti inayosikika pale wanapokemea maovu badala ya kujichanganya katika mambo yanayoshusha hadhi yao na hivyo kupoteza nguvu za kutoa maagizo au makalipio.
Akizungumza na viongozi hao Mkuu wa Wilaya hiyo Ndugu Joseph Mkude aliwashukuru kwa kukubali wito wake akiahidi kuimarisha mahusiano ili waweze kushiriki katika kutekeleza mipango mbalimbali ya serikali.
“Ndugu wazee wangu na wajumbe wote natambua michango yenu, nilikuwa natafuta namna ya kuonana nanyi kwa muda mrefu,leo nafurahia kuwa pamoja nanyi ili tuweze kujadili namna nzuri ya kushirikiana katika kujenga wilaya yetu”alisema kiongozi huyo.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuwathamini na kuwatumia katika kupiga vita maovu katika jamii ikiwemo migogoro ya kifamilia,pamoja na waganga wapiga ramli (maarufu kama rambaramba)ambao wamekuwa wakijitokeza wilayani humo wakishawishi jamii kuwapa kazi ya kutoa dawa za kichawi kwenye makazi ya watu.
Machifu kwa upande wao waliiomba serikali na jamii kwa ujumla kuendelea kuwathamini kwa vile wana majukumu mengi wanayoyafanya ya ujenzi wa jamii lakini yamekuwa yakipuuzwa na baadhi ya watu hasa hawa vijana hawa wa kizazi kipya.
Ikumbukwe kuwa,MUJATA hujumuisha viongozi wa dini,machifu ,waganga wa tiba mbadala pamoja na wajumbe wengine wa kuchaguliwa kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya.
Uchunguzi umebaini juu ya uwepo wa misitu yenye miti ya asili inayotunzwa kimila ikiwa inatumika katika shughuli za tambiko ikiwemo ya wa ukoo wa Kibona katika Kata ya Kalembo,ukoo wa Kabuje katika Kijiji cha Lusalala pamoja na ukoo wa Musomba kule Kata ya Malangali.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa