Ileje-Songwe
Vijana wa rika balehe wilayani Ileje wametakiwa kujenga misingi ya tabia njema ili kufikia ndoto zao na kuepukana na vitendo visivyokubalika katika jamii.
Vijana hao wenye umri kati ya miaka 15-19 walipewa ujumbe huo wakati wa kikao cha siku moja kilichofanyika mjini Itumba kikitathimini matokeo na changamoto za Programu ya Ongea Redio inayolenga kupunguza maaambukizi ya VVU na UKIMWI.
Akizungumza na vijana wapatao 20 ambao ni viongozi vya klabu za shuleni na mtaani msimamizi wa program hiyo Ndg.Faustina Mwenda alisema mradi huo hauna budi kuleta matokeo chanya katika maeneo ambayo kuna klabu hizo bila kuathiri makundi ya aina hiyo yanayopambana na maambukizi ya VVU Na UKIMWI kama vile FEMA.
Alisema kuwa,elimu wanayoipata iwe kinga dhidi ya maadui wanaotaka kukwamisha ndoto zao ili taifa liweze kuwa na viongozi wenye afya njema na tabia nzuri.
Akizungumzia mradi huo Afisa Elimu Taaluma kwa shule za sekondari Mwl.Elimu Kaminyoge aliwataka wanafunzi kuwa makini katika matumizi ya teknolojia ili kuepuka yale yanayoweza kuwaharibia tabia.
Kwa upande wao vijana hao,walieleza changamoto wanazokabiliana nazo katika kutekeleza program hiyo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa mtandao wa simu wa kutosha katika baadhi ya maeneo.
Tatizo lingine ni mwingiliano wa ratiba zikiwemo za masomo kwa makundi ya shuleni pamoja na kupangiwa majukumu na wazazi kwa makundi ya uraiani.
Hata hivyo,mradi huo ulishindwa kuyafikia maeneo yote ya wilaya kwasababu ya kutofikiwa na masafa ya Redio ya Kijamii ya Ileje FM ambayo hurusha vipindi vya mradi huu pamoja na ufinyu wa bajeti kwa wafuatiliaji iwapo maeneo ya mbali na Makao Makuu ya Wilaya yangehusishwa.
Naye Mratibu wa Kuthibiti UKIMWI wilayani humo Ndg.David Gunza alisema kuwa mradi huo ungefanya vizuri zaidi kama ungekuwa na maandalizi ya kutosha na kuhusisha watu wengi kwani mradi huu haukuwa na maandalizi ya kutosh,hivyo ichukuliwe kama changamoto itakayoleta fursa kwa kipindi kijacho.
Ongea Redio inafanyakazi kazi katika Halmashauri nane kwa Tanzania Bara na Mikoa yote ya Tanzania Visiwani ikishirikiana na Tume ya Kuthibiti UKIMWI kwa Tanzania Bara,Tume ya UKIMWI Zanzibar pamoja na UNICEF.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa