Wilaya za Ileje ya Tanzania na Chitipa ya Malawi zimefanya kikao cha ujirani mwema kujadili namna ya kukabiliana na ebola iwapo inaweza kutokea.
Kikao hicho cha siku moja kilifanyika katika Ukumbi wa VIM uliopo Itumba Ileje kiliwakutanisha Wakuu wa Wilaya,wajumbe wa Kamati za ulinzi na usalama na Wakuu wa idara wa pande zote mbili.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje Ndg.Joseph Mkude alisema kuwa kikao hicho kililenga kubadilishana uzoefu wa namna kila upande ulivyojipanga katika kukabiliana na ugonjwa wa ebola pindi unapoweza kutokea.
Alisema kuwa kumekuwa na mwingilano mkubwa kati ya wananchi wa pande hizo mbili kiasi kwamba upande mmoja utakapoathirika upande mwengine hauwezi kusalimika.
Humfrey Gondwe Mkuu wa Wilaya ya Chitipa Malawi aliwataka wajumbe kuwa na mikakati ya kukabiliana na ebola inayolenga kulinda utu wa mwafrika kama alivyokuwa akihimiza Hayati Mwl.J.K.Nyerere mwasisi wa Taifa la Tanzania.
Alisema kuwa Hayati Nyerere alikuwa kiongozi aliyeweza kuzipa kipaumbele shida za waafrika bila kujali mipaka akisema vita dhidi ya ebola ni ya waafrika wote.
Kikao hicho kiliweza kupokea taarifa kutoka kwa watalaam wa afya na makubaliano yalikuwa kila upande kwenda kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kwa kuhusisha makundi mbalimbali katika jamii kuhusu ugonjwa wa ebola.
Pamoja na mambo mengine Wamalawi waliendelea kuipongeza serikali ya Tanzania kwa ujenzi wa barabara ya Mpemba hadi Isongole kwa kiwango cha lami wakisema kuwa itaongeza kasi ya maendeleo kwa wanachi wa pande hizo mbili.
Mhe.Nick Masebo Mbunge wa Jimbo la Chitipa North alisema kuwa hatua iliyofikiwa na Tanzania katika ujenzi wa barabara hiyo ni changamoto kwao hivyo kisiasa kuna mkakati wa kuunganisha barabara hiyo.
Kwa muda mrefu wilaya hizo zimekuwa zikikutana katika kujadili namna ya kuufanya mpaka huo kuwa makazi salama kwa raia wa pande.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni,Mhe.Rais Magufuli alifanya ziara nchini Malawi na kuongeza kasi ya mahusiano ya kihistoria kwa mataifa haya mawili ambayo watu wa mpakani wanafanana kwa lugha zao.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa