Bi.Mary Alois Afisa Lishe wa Wilaya hiyo alisema kuwa katika maadhimisho hayo zaidi ya watoto 85 wakiwa wameambatana na wazazi na walezi wao walifika katika Ofisi za Kijiji hicho waliweza kupimwa ambapo watoto 20 kati yao walibainika kuwa na dosari za ukuaji
Afisa huyo aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanazingatia suala la lishe na kulifanya kuwa agenda ya familia ili kuepusha udumavu unaowakabiri watoto wengi wa mkoa wa Songwe licha ya kuwa na uzalishaji wa vyakula vya aina mbalimbali.
Naye Anna Mwakipesile kutoka Hospitali ya Itumba aliwataka wazazi kuzingatia lishe bora kwa mama wajawazito kwa vile mama mjamzito akikosa lishe bora madhara huwa makubwa kwa mtoto aliyeko tumboni
Hata hata hivyo,mahudhurio ya wanaume katika tukio hilo hayakuwa ya kuridhisha kwani wanaume wachache tu waliokuwepo huku wakiwa ni wale wenye majukumu maalum.
Bi.Neema Mwenga mmoja wa wazazi walioshiriki katika tukio hilo alikiri juu ya kuwepo kwa elimu ya lishe ya kutosha ambayo alisema kuwa huipata kupitia Wahudumu wa Afya Vijijini ,wakati wa kuhudhuria kliniki pamoja na kutoka kwa watalaam wa wilayani.
Alisema kuwa tatizo huwa ni wakati wa utekelezaji kati ya mtu mmoja mmoja kulingana na tabia ya mtu binafsi ambapo alisema kuna wengine huendekeze masuala ya ulevi badala ya kutoa kipaumbele cha lishe kwa familia.
Solomon Kandonga Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho alikiri kuwapo kwa tatizo hilo baada ya kubainika kwa watoto hao 20 wenye dosari za ukuaji akiahidi kulichukulia kwa uzito ikiwemo kutekeleza maagizo ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii yanayowataka viongozi wa eneo husika kufanya ufuatiliaji.
Maadhimisho kama hayo tayari yamefanyika katika vijiji vya Ibeta,Kikota na Mlale yakitarajiwa kuendelea katika vijiji vingine kwa kutoa elimu,kujua ukuaji wa watoto na kutoa ushauri kwa wazazi na walezi wa watoto wanaobainika kuwa na dosari za ukuaji.
Mkoa wa Songwe ulishaanza kampeni ya kukomesha udumavu kwa watoto unaosababishwa na kukosa lishe bora huku halmashauri zote za wilaya pamoja na wadau wengine wakitakiwa kushirikiana ili kufikia lengo hilo.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa