Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Ileje Mkoani Songwe Ndg.Geofrey Nnauye ameshakabidhi ofisi kwa Bi.Nuru Kindamba ambaye ni Mkurugenzi Mpya wa halmashauri hiyo .
Makabidhiano hayo yamekuja yakiwa ni matokeo ya uteuzi wa wakurugenzi watendaji pamoja na uhamisho kwa wengine ambapo Nnauye amehamia kuwa Mkurugenzi wa Mji wa Newala nafasi yake ikichukuliwa na Bi.Nuru Kindamba aliyeteuliwa kwa nafasi hiyo.
Akizungumza baada ya kukabidhi halmashauri nzima Nnauye aliwashukuru viongozi wote wa wilaya pamoja na wananchi wote kwa jinsi walivyompa ushirikiano katika muda wake huku akikiri juu ya ugumu wa nafasi hiyo nyeti katika mamlaka za zerikali za mitaa iwapo hekima,ushirikishwaji na uvumilivu hauwezi kupewa nafasi.
Katika muda wake amefanya mambo kadhaa ambayo viongozi wengine akiwemo Mkuu wa Wilaya pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri wanakiri kuwa aliyapigania kwa nguvu zake zote ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule ya wasichana ya Ileje,ghala la mazao linalojengwa kwa mapato ya ndani katika Kijiji cha Isongole,pamoja na utafutaji na ununuzi wa magari mapya ambapo sasa hali si mbaya.
Naye Mkurugenzi mpya wa halmashauri hiyo Bi.Nuru Kindamba ameshukuru kwa mapokezi aliyoyapata tangu kuwasili kwake wilayani humo huku akiahidi kufanya kazi sawa na miongozo ya nafasi yake hiyo huku akiomba ushirikiano uliokuwepo kwa DED anayeondoka uendelezwe kwake pia.
Akizungumza katika kikao hicho cha makabidhiano Mhe.Ubatizo Songa ambaye ni shuhuda wa lazima kisheria aliahidi kuendelea kufanya kazi bega kwa bega na Mkurugenzi huyu mpya katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mabadiliko haya kwa wilaya ya Ileje yamefanyika pia kwa upande wa serikali Kuu ambapo Katibu Tawala amekuwa mpya yaani Ndg.Abdallah Ramadhan Mayombo akichukua nafasi ya Ndg.Mathias Mizengo.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa