Mhe.Farida Mgomi Mkuu mpya wa Wilaya hiyo akikabidhiwa wilaya hiyo kwa maandishi kutoka kwa Mhe.Anna Gidarya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo aliombwa kuangalia kwa jicho la pekee shule hiyo mpya iliyopo kaktika Kata ya Chitete akieleza kuwa alikuwa ameiwekea nadhiri kuhakikisha inakuwa chachu ya ukombozi wa mtoto wa kike wilayani humo.
Mhe.Gidarya aliyehamishiwa wilaya ya Busega alimwomba mkuu huyo wa wilaya kuendeleza juhudi za kuwasaidia watoto wa kike kupitia shule hiyo pekee ya kike wilayani humo.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo Mhe.Mgomi ameshukuru kwa kuaminiwa na Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Kiranja Mkuu wa watumishi wote wilayani humo
Aliongeza kuwa peke yake kamwe hawezi kuiendeleza wilaya isipokuwa kwa umoja,ushirikiano na mshikamano baina yake,viongozi wengine na wananchi kwa ujumla.
Mhe.Mohamed Mwala Diwani wa Kata ya Itumba akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya aliunga kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe.Waziri Kindamba aliyoitoa wakati wa kuwaapisha Wakuu wa Wilaya kwa niaba ya Mhe.Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan juu ya kujiepusha kurithi maadui
Alisema kuwa nafasi zao za kazi hazina budi kuzingatia weredi na imani kwa Mhe.Rais wakati wa kuwatumikia wananchi pasipo kuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika ofisi za Mkuu wa Wilaya zilizopo Itumba yakishuhudiwa na vingozi mbalimbali wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM)
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa