Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Ileje imekagua Miradi ya Maendeleo inayoendelea kutekelezwa huku ikikerwa na huduma zinavyotolewa katika Hospitali ya Wilaya pamoja na Shirika la Umeme TANESCO linavyolalamikiwa na wananchi.
Wakiwa kwenye ukaguzi wa Ujenzi wa Hospitali ya wilaya hiyo viongozi hao walifurahishwa na hatua za ujenzi huku wakiwataka watendaji kukamilisha hatua zilizobaki ili wananchi waweze kupata huduma badala ya kuendelea kuyaangalia majengo yasiyotumika.
Hata hivyo furaha yao ilikatishwa na kukosekana kwa mashuka katika wodi ya wazazi ambapo walishuhudia vikoi na vitenge vikitumika badala ya mashuka huku wahusika wakitoa sababu ambazo hazikuwaridhisha wajumbe.
Hali hiyo,ilitokea pale wajumbe walipoingia wodi ya wazazi ili kuwajulia hali kinamama waliojifungua ambapo waliweza kutoa fedha tasilimu elfu 27,000.
Wakiwa katika Kijiji cha Isongole ambako walifuatilia kukosekana kwa umeme tangu tarehe 3/1 /2020 viongozi hao toka chama Tawala walielezwa na wakazi wa Isongole kuwa baadhi ya watumishi wa TANESCO Wilayani humo wamekuwa wakitoa huduma kwa kutengeneza mazingira ya rushwa.
Akijibu tuhuma hizo,meneja wa Shirika hilo Ndg.James Bigambo aliahidi kulifanyia kazi suala hilo ambalo ni kero ni kinyume na Ilani ya Chama cha Mapinduzi inayowataka watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa wananchi pasipo kuzalisha kero.
Wakiwa kwenye ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya maadarasa katika Sekondari ya Mbebe walionya viongozi wa Kata akiwemo diwani wa kata hiyo Mhe.Chaghi Kalinga na Mtendaji wa Kata kwa kushindwa kuwaunganisha wananchi na kuwahamasisha kushiriki ujenzi wa darasa ili likamilike kwa wakati
Pia Kamati hiyo ilimtaka Meneja wa TARULA wa Wilaya kuhakiisha anasimamia vema ukarabati wa barabara ya Mlale-Chitete baada ya dosari kadha kubainika zikioneshwa kazi kufanywa chini ya viwango.
Akizungumza wakati wa majumuisho ya ziara hiyo Mwenyekiti wa C.C.M wa Wilaya hiyo Ndg.Hebron Kibona aliwataka watendaji wa serikali kuhakikisha miradi yote inatoa huduma huduma bora kwa wananchi ambao chama kina mkataba nao kwa miaka mitano.
Ziara hiyo,ambayo hufanyika kila robo ya mwaka ilijumuisha pia Mkuu wa Wilaya Ndg.Joseph Mkude Katibu Tawala wa Wilaya Ndg.Matias Mizengo,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na Wakuu wa Idara.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa