Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Tawi la Tunduma, imekabidhi Msaada wa Magodoro 16 yenye thamani ya Shilingi Laki nne na Elfu Themanini (480,00/=) katika Gereza la Wilaya ya Ileje lililopo katika kata ya Itumba wilayani hapa.
Msaada huo umekabidhiwa mapema leo Januari 30,2025 na Meneja wa NBC Tawi la Tunduma Bw. Shedrack Mpanda ambaye aliambatana pamoja na Timu ya wafanyakazi wa Benki hiyo kutokaTunduma ikiwa ni sehemu mojawapo ya benki hiyo katika kuimarisha Mahusiano na Ushirikiano hasa kwa kuigusa jamii na makundi yenye uhitaji ikiwemo wafungwa katika Magereza.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo meneja wa Benki ya NBC, alisema Msaada huo ni sehemu ya Jitihada za wafanyakazi wa NBC katika kuyagusa makundi maalumu katika jamii sambamba na kuwatia moyo pale walipokata tamaa ili wazidi kusonga mbele na kujiona kuwa ni sehemu mojawapo katika Jamii.
Akizungumza mara baada ya kupokelewa kwa msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mheshimiwa Farida Mgomi, ameishukuru Benki ya NBC kwa kuwa sehemu mojawapo ya Faraja kwa wafungwa wa Gereza la Ileje kupitia msaada wa magodoro waliyoyatoa siku ya leo. Aidha ameipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kufanya matendo ya huruma yanayoigusa Jamii na Makundi maalumu pamoja na kuwasihi kuendelea kuwa na utamaduni huohuo wa kuigusa Jamii.
Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Ileje , Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Alfred Peter Chimachi ameishukuru benki ya NBCkwa kutoa msaada huo wa magodoro sambamba na kutoa rai kwa wafungwa kuyatunza magodoro hayo vizuri.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa