Katika jitihada za kuendeleza shughuli za Kiuchumi na kulinda Mazingira, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje,Frank Kisanga kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje , amekabidhi Msaada wa Mizinga 95 ya kufugia nyuki kwa vikundi vya Maendeleo katika Kata ya Malangali wilayani hapa.
Msaada huo unaofadhiliwa na Joint Songwe River Basin Commission, shirika linalojihusisha na usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji na mazingira katika bonde la mto huo. umekabidhiwa mapema leo April 25,2025 huku Lengo kuu likiwa ni kuwawezesha Wananchi Kiuchumi kwa njia endelevu kupitia shughuli za Ufugaji nyuki, ambazo huchangia pia katika utunzaji wa mazingira.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Afisa Mazingira alisema kuwa ufugaji nyuki ni mojawapo ya njia bora ya kuongeza kipato kwa jamii, hasa kwa maeneo ya vijijini, huku pia ikisaidia kuhifadhi mazingira kwa kuhamasisha upandaji miti na kutunza misitu. Alisisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kushirikiana na Mashirika ya Maendeleo kama Joint Songwe River Basin Commission ili kuleta maendeleo kwa Wananchi wake.
Katika hatua nyingine ,Kisanga aliwataka wanavikundi wanaopokea mizinga hiyo kuitunza kwa matumizi sahihi, kwa kuhakikisha kuwa wanaitumia kama njia ya kujiletea maendeleo na si vinginevyo. Alitoa wito wa usimamizi madhubuti wa mizinga hiyo ili iweze kutoa matokeo chanya kwa muda mrefu.
Kwa upande wao, baadhi ya wanavikundi walioshuhudia makabidhiano hayo walitoa shukrani kwa Halmashauri na Wafadhili kwa Msaada huo, huku wakiahidi kuutumia kama kichocheo cha mabadiliko chanya ya kiuchumi kwao na jamii zao kwa ujumla. Msaada huu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuinua hali ya maisha ya wananchi wa Kata ya Malangali, sambamba na kuchangia juhudi za kulinda mazingira ya Bonde la Mto Songwe.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa