ZAO LA KAHAWA KWA WILAYA YA ILEJE
TAREHE 17/04/2020.
UTANGULIZI.
Wilaya ya Ileje ipo upande wa Kusini Mashariki mwa Mkoa wa Songwe, na ina eneo la kilomita za mraba 1908. Kiutawala wilaya ya Ileje imegawanyika katika tarafa mbili ambazo ni Bulambya na Bundali kuna jumla ya kata 18, vijiji 71, vitongoji 317 na jumla ya kaya zinazojihusisha na kilimo ni kaya 32,160, zinazojihusisha na kilimo cha kahawa ni kaya 3,154.
ZAO LA KAHAWA.
Kahawa ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayolimwa katika wilaya ya Ileje tarafa ya Bundali kwenye kata za Sange, Kafule, Ikinga, Malangali, Kalembo, Luswisi, Lubanda na Nguluguru na kwa Tarafa ya Bulambya Kahawa inalimwa katika kata za Itale na Ibaba.
Malengo kwa mwaka 2019/2020 yalikua ni hekta 7070 na malengo ya uzalishaji yalikuwa ni tani 875 na utekelezaji ulikuwa ni hekta 6234 na uzalishaji uliofikiwa ni tani 716.58.
JUHUDI ZA WILAYA KATIKA KUENDELEZA ZAO LA KAHAWA.
Msimu wa 2019/2020, halmashauri imenunua kilo 90 za mbegu ya kahawa aina ya Compact na kuisambaza katika kata zinazolima zao la kahawa ili zikazalishe miche ambayo itagawanywa kwa wakulima wa kahawa katika vikundi vinavyojishughulisha na uzalishaji wa kahawa. Hivyo jumla ya miche 262,000 inategemewa kuzalishwa.
Kupitia Maafisa Ugani mafunzo yametolewa kwa wakulima ili kuongeza ubora wa Kahawa katika kuzingatia hatua za uvunaji na namna ya kukausha kahawa ili kufanya kahawa isipoteze ubora pia kutumia mitambo ya kati katika kumenya Kahawa.
Kutekeleza maelekezo ya mabadiliko ya uuzaji wa kahawa kupitia vyama vya ushirika (AMCOS) kwa msimu wa 2019/20.
Uundwaji na uimarishaji wa vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) katika ngazi ya kata, mpaka sasa kwa wilaya ya Ileje tumeunda Amcos kumi na tano (15) zinazojihusisha na uzalishaji, ukusanyaji na usafirishaji wa kahawa kwenda kwenye viwanda vya ukoboaji. Ambavyo ni MCCCO Campany Ltd, GDM Company Ltd, CMS Company Ltd na City Coffee Company Ltd.
Uhamasishaji wa vyama vya ushirika ili kuwa na mitambo ya kati ya kuchakata kahawa inayotoka shambani (CPU) kwa lengo la kuongeza ubora wa kahawa unafanyika ambapo mpaka sasa tuna jumla ya CPU 6.
CHANGAMOTO ZA TASNIA YA KAHAWA.
Mabadiliko ya tabia ya nchi (hali ya hewa) yanayopelekea uzalishaji wa zao la kahawa kushuka.
Uhaba wa wataalamu wa kilimo katika baadhi ya kata na vijiji watakaotumiwa na wakulima wa kahawa kwa ajili ya ushauri, kutoa elimu na kusimamia shughuli mbalimbali zinazoendelea katika mashamba ya wakulima wa kahawa.
Kukosekana kwa Mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa kilimo (Maafisa Ugani) kuhusu teknolojia mpya ya uzalishaji wa zao la Kahawa.
UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA TASNIA YA KAHAWA.
Vyama vya Ushirika vya mazao (AMCOS) vimeshauriwa kukopa mikopo ya muda mfupi na yenye riba nafuu ya mwaka mmoja ili kuweza kuongeza nguvu katika kutoa huduma kama malipo ya awali kwa wakulima. Pia wana AMCOS wameshauriwa kujiunga na kuweka Akiba kwenye vyama vya akiba na mikopo SACCOS vya maeneo yao ili kuepuka kuwa na changamoto ya fedha za kuchumia kahawa na pembejeo kwa msimu unaofuata.
Kuboresha miundombinu ya hifadhi ya mazao ya wakulima kwenye vyama vyao. (kujenga maghala, kukarabati maghala mabovu kwa kutenga kiasi cha fedha kila wanapouza kahawa).
Kulima kilimo cha zao la kahawa kinachozingatia mabadiliko ya tabia ya nchi ili kuongeza uzalishaji na kukabiliana na changamoto za hali ya hewa zinazoweza kujitokeza mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kutumia mbegu zenye ukinzani na magonjwa kama Compact, kufuata kanuni bora za uzalishaji .
Kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara wataalamu wa kilimo (Maafisa Ugani) kuhusu kanuni bora na teknolojia mpya ya uzalishaji wa zao la Kahawa ili kuwajengea uwezo wa kutoa elimu na kuongeza uzalishaji kwa wakulima wa kahawa.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa