Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Bi. Nuru Waziri Kindamba ametoa rai kwa Watumishi Wapya wa Wilaya yetu kuzingatia Maadili, Weledi, Ubunifu, Nidhamu na Ufanisi katika kutekeleza majukumu ya kazi waliyopangiwa katika wilaya hii.
Akizungumza wakati wa Semina ya Mafunzo kwa Watumishi Wapya wa Kada mbalimbali katika Halmashauri hii iliyofanyika katika Ukumbi wa RM mapema leo February 25, 2025, Bi. Kindamba amewasisistiza watumishi hao kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuwa na Nidhamu ya kazi ili kufanikisha Ustawi wa Wananchi katika Wilaya ya Ileje.
Aidha amewaasa watumishi hao kuimarisha mahusiano mema baina yao na wananchi, sambamba na kuepuka vitendo vya Rushwa na Ubadhirifu wa Fedha za Serikali, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanasimamia vyema Miradi mbalimbali ya Serikali inayotekelezwa katika Wilaya hii pamoja na kusimamia Ukusanyaji wa Mapato ili kuleta tija kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hii amewaasa watumishi hao kuzingatia umoja, ushirikiano na mshikamano hii ikiwa ni pamoja na kusaidiana katika Shida na Raha pamoja na kuchangamkia Fursa za Kiuchumi zilizopo wilayani hapa ili kujiimarishia kipato mbali na Mshahara.
Semina ya mafunzo kwa Watumishi wapya katika Halmashauri ya Wilaya hii inalenga kuwajengea uwezo na kutoa miongozo ya kazi ili watumishi ili kuepuka vitendo visivyokuwa na maadili na utovu wa nidhamu pamoja na kuitambua mipaka na Miongozo ya kazi.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa