Na:Daniel Mwambene IlejeDC
Serikali imeonya watendaji wake wa mpakani wanaokwamisha Diplomasia ya Uchumi huku ikikasirishwa na ukusanyaji duni wa mapato pamoja na kukosekana kwa takwimu sahihi zinazohusu mpaka wa Isongole –Ileje Tanzania na Mbilima-Chitipa nchini Malawi.
Onyo hilo lilitolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya nchi za nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Damas Ndumbalo wakati wa ziara ya siku moja aliyoifanya wilayani humo iliyomwezesha kufika hadi eneo la mpaka wa Tanzania na Malawi na kuzungumza na wajasiliamali.
Akiwa kwenye Ofisi za Forodha Kituo cha Isongole Waziri huyo hakufurahishwa na utendaji kazi wa mazoea uliooneshwa na watendaji kupitia taarifa yao ikiwa na makisio na makusanyo madogo kwa mwezi huku takwimu zake zikiwa hazioneshi uhalisia.
Alisema kuwa juhudi kubwa zinazofanywa na serikali katika kuanzisha viwanda na kuboresha miundombinu hazitakuwa na maana iwapo mipaka ya nchi haitaongeza mapato kutokana na biashara za mpakani ambapo wafanyabiashara wengi toka nchini Malawi wamekuwa wanunuzi wakuu wa bidhaa za madukani toka Tanzania.
Dk.Ndumbalo aliongeza kuwa ujenzi wa Barabara ya Isongole- Mpemba kwa kiwango cha lami hautakuwa na maana iwapo watendaji wake watakosa ubunifu na weredi katika kushauri serikali kubaini fursa za biashara mpakani.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Ileje Ndg. Joseph Mkude alimweleza Waziri huyo kuwa licha ya kuwepo kwa mahusiano makubwa na Wilaya ya Chitipa-Malawi bado kuna changamoto kadhaa kama vile kuhamahama kwa Mto.Songwe ambao ni mpaka wa nchi hizo mbili eneo la Navilolo katika Kijiji cha Ikumbilo nchini Tanzania.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe.Benedicto Mashiba alisema kuwa wamekuwa wakipokea kero mbalimbali toka kwa wafanyabiashara wa Malawi wanaotumia mpaka huo zikidaiwa kusababishwa na watendaji wa serikali wanaokosa uadilifu.
Baadhi ya raia wa Malawi waliokutwa mpakani hapo wakisafirisha mazao walimweleza Mhe.Waziri namna wanavyonufaika na mpaka huo na kutegemeana katika mambo mbalimbali kama biashara ya pembejeo na mazao ya nafaka.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa