Wananchi wilayani Ileje wamesherehekea Siku ya Muungano mwaka huu kwa kuvamia Hospitali ya Wilaya hiyo wakiwa na majembe,sululu,sepetu na ndoo wakiuunga juhudi za serikali katika kuwaletea wananachi maendeleo.
Wakazi hao wakiongozwa na viongozi wao wa Serikali za Kata za Itumba,Isomgole,Ndola na Mlale waliweza kufikia hatua hiyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea wananachi maendeleo yao baada ya Serilkali chini ya Mhe.Rais Magufuli kumwaga bilioni moja na milioni 500 kwaajili ya ujenzi huo.
Hapo awali Mkuu wa Wilaya hiyo Ndugu Joseph Mkude alitoa wito kwa wanachi kusherehekea Siku ya Muungano kwa kushiriki ujenzi wa hospitali hiyo hali iliyoonekana kuungwa mkono kwa mahudhurio makubwa.
Katika zoezi hilo lililochukua takribani masaa matatu lilihusu uchimbaji msingi kwa majengo yote manne,usombaji wa mchanga na uhamishaji wa bomba maji.
Upanuzi na ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya utakapokamilika unatarajiwa kuwa mkombozi kwa wananchi hao ambao hapo awali walikuwa wakisafiri zaidi ya kilometa 60 hadi hospitali ya Kanisa la Moraviani ya Isoko pamoja na kwenda kutibiwa nchi jirani ya Malawi.
Mzee Nsajigwa Kibona mmoja wa wakazi wa Itumba alisema kuwa kwa miaka zaidi ya 50 aliyoishi hapo ameona mabadiliko makubwa katika hosiptali hiyo akiamini kuwa yatakwenda sanjali na ubora wa tiba.
Wilaya ya Ileje ina miradi kadhaa ya ujenzi vikiwemo vituo vya afya vya Ibaba na Lubanda pamoja na zahanati katika vijiji mbalimbali vikiwemo vya Izuba,Bwenda Mapogoro na Ilulu.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa