Wakulima wa zao la pareto Wilayani Ileje mkoani Songwe wameiomba serikali kuingilia kati juu ya bei isiyozingatia gharama za uzalishaji ili waendelee kuzalisha kwa tija.
Kilio hicho kilitolewa na wakulima wa zao hilo katika Kata ya Itale wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya hiyo Ndugu Joseph Mkude wakisema kuwa bei ya zao hilo imedumaa.
Mzee Philimon Ndidi mmoja wa wakulima hao alisema kuwa bei hiyo imekuwa haipandi kwa muda mrefu.
“Mhe.Mkuu wa Wilaya huyu mnunuzi wa pareto hajawahi kupandisha bei zaidi ya shilingi 2300/= za kitanzania kwa kilo,bali amekuwa akishusha na kupandisha hadi bei hiyo kila wakati,tunaomba tusaidie kiongozi wetu”alisema Mzee huyo.
Wakulima wengine waliongeza kuwa kata hiyo haijanufaika vya kutosha kutokana na uzalishaji ulivyo mgumu ambapo kinachovunwa ni maua ambayo hadi kufikisha kilo moja inakuwa gharama kubwa.
Akizungumza na wakulima hao kiongozi hiyo aliwaahidi kulifanyia kazi na kuwapa mrejesho akiwataka kutovunjika moyo katika uzalishaji na kujiunga katika vikundi ili kuwa na sauti moja ya kuwatetea.
“Unganeni ndipo serikali inaweza kuwaona kwa urahisi na mtakuwa na uwezo wa kupaza sauti hadi mbali zaidi badala ya kila mmoja kujipigania.
Hali ikiwa hivyo huko Itale Idara ya Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika Wilayani humo kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao hilo imekuwa ikifanya juhudi katika kuongeza uzalishaji kwa kuhamasisha kuanzisha mashamba mapya katika Kata ya Lubanda katika Kijiji cha Mbembati.
Afisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika Ndugu Herman Njeje akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake alisema kuwa wanashikiana na “ Pyrethrum Company of Tanzania Ltd “ (PCT) katika kuendeleza zao hilo wilayani humo.
Kuhusu bei kutopanda Afisa huyo alipinga akisema kuwa kinachoogeza bei ya zao hilo si muda bali ni ubora wake ambao umepangwa kulingana na wingi wa sumu iliyomo katika zao hilo ambayo hutokana na maandalizi tangu shambani hadi inapopelekwa sokoni.
Kuhusu kudorola kwa soko la matunda aina ya maparachichi yanayozalishwa katika kata za ndola na Itale Ndg. Njeje alisema kuwa ambao ni Kuza Africa,Rungwe Avocado na Lima Kwanza wamechelewa kwenda kwa wakulima kununua zao hilo kutokana na changamoto za kibiashara.
Amesema kuwa Idara yake inahaha huku na huko kuhakikisha wakulima hao wanauza zao hilo kwa njia yoyote ilimradi wasiweze kupata hasara na kukata tama ya kuendelea kuzalisha.
Alisema kuwa,bei hiyo hupangwa kwa madaraja kuanzia I hadi VI ambapo daraja la I hutakiwa kuwa na sumu 1.8%-1.89% huuzwa kwa Tzsh 3100/= na daraja la VI lenye kiwango cha sumu 0.90% huuzwa Tzsh 1500/= kwa kilo.
Wilaya ya Ileje ni miongoni mwa wilaya za Nyanda za Juu Kusini zinazozalisha zao la pareto katika Kata za Itale,Ibaba,Ngulilo,Ndola na Lubanda kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa zao hili linalotumika kutengenezea sumu,soko lake limeanza kupata changamoto kutokana na teknolojia inavyokuwa duniani katika matumizi mbadala ya sumu inayotokana na pareto.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa