Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Mkoani Songwe kimepongeza serikali ya Awamu ya Tano kwa kutopunguza mishahara ya watumishi wa umma wakati huu wa janga la Korona kama yalivyofanya mataifa mengine.
Hosea Yusto Katibu wa Chama hicho alitoa pongezi hizo kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakati wa kikao cha siku moja alipokuwa akizungumza na wanachama toka Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wakati wa kugawa tesheti na kofia ambazo zingetumika kwenye maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu
Hosea alisema kuwa wakati baadhi ya mataifa Duniani yamepunguza mishahara ya watumishi ili kuelekeza nguvu katika mapambano dhidi ya gonjwa la Covid-19 serikali ya Tanzania haijafanya hivyo hali iliyosaidia kutoathiri maisha ya wafanyakazi,hivyo kuendelea na mipango yao ya kila siku.
Aliongeza kuwa kwa muda mrefu serikali haijatoa nyongeza za mishahara kwa watumishi wake kwa kuwa ilikuwa ikirekebisha mwachano mkubwa uliokuwepo baadhi wakipata zaidi ya milioni 30 huku wangine wakiambulia fedha kidogo wakati wote ni watumishi wa umma.
Kwa upande wao wananchama waliomba uongozi wa mkoa huo kuwa na uwezo wa kuchukua hatua za haraka kutetea haki za watumishi yakiwemo masuala ya kupanda vyeo kwa wenye sifa pamoja na kubadilishiwa mishahara kwa wakati.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndg.Haji Mnasi alisema kuwa ataendelea kushirikiana na TALGWU katika kuhakikisha kuwa watumishi wa umma walio chini yake wanatatuliwa changamoto zao,hivyo kufanya kazi kwa ufanisi ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa