Taifa linaangamia kwa UKIMWI kwasababu ya unafiki-RC Chalamila.
Mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI likiwa ni moja ya malengo ya kitaifa,Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Ndugu Albert Chalamila ameitaka jamii kuacha unafiki ili kufikia malengo hao.
Akizindua Mpango wa Ongea Radio Programu kwa mikoa ya Nyanda za juu Kusini katika ukumbi wa Tughimbe Jijini Mbeya RC huyo alisema kuwa UKIMWI umekuwa huutokomei kwakuwa wadau mbalimbali wa vita hivi wanashindwa kukiishi kile wanachokisema majukwaani.
Alisema kuwa,unafiki kwa wadau mbalimbali ndilo tatizo linalokwamisha tusishinde kwa wakati mapambano hayo kwakuwa sehemu kubwa ya jamii inaendekeza ngono ambayo njia kuu inayoeneza VVU na Ukimwi.
Alisema kuwa ili kuokoa kizazi kijacho jamii haina budi kutumia nguvu katika kuokoa vijana ambao ni wahanga wakuu wa janga hili ambalo limeshapoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa na Dunia nzima kwa ujumla.
Aliongeza kuwa mikoa ya Iringa,Mbeya,Njombe na Songwe imelengwa kwakuwa ina maambukizi makubwa kuliko maeneo mengine akiahidi kushirikiana na Wakuu wa Mikoa ya Kanda hiyo katika mapambano yenye kuleta matokeo chanya.
Grolia Kyando mwanafunzi wa Kidato Cha Pili toka Sekondari ya Buliaga Wilayani Rungwe aliyeshiriki uzinduzi wa zoezi hilo alisema kuwa atahakikisha anawajengea ujasiri wanafunzi wenzake wa kike katika kuepukana na vishawishi vinavyoweza kuwasababishia mimba za utotoni.
Ongea Redio Programu ni mpango unaoratibiwa na UNICEF kwa ushirikiano na TACAIDS pamoja TAMISEM ukiwalenga vijana wa miaka 15 hadi 19 katika masuala ya kujikinga dhidi ya VVU na UKIMWI,Elimu ya Afya ya Uzazi pamoja na jinsi ya kuepuka na mimba za utotoni.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa