RC wa Songwe atembelea vivutio vya utalii wilayani Ileje afurahishwa na Mradi wa Shamba la Iyondo-Mswima akihimiza kulindwa kwa misitu ya asili iliyopo wilayani humo asherehekea siku yake ya kuzaliwa katika vilele vya milima ya shamba hilo.
Ukiwa ni mwisho wa juma siku ya Jumamosi Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemas Mwangela alitembelea vivutio vya utalii vilivyopo wilayani Ileje ikiwa ni sehemu ya utalii wa ndani kwa timu nzima aliyokuwa amefuatana nayo.
Ziara hiyo ya siku moja ilimwezesha kufika hadi Kijiji cha Ndembo mahali panapozalishwa nyungo zitokanazo na mianzi ambapo aliweza kukutana na wasukaji akiwahimiza kuungana katika vikundi ili kuweza kutambuliwa na serikali na kuongeza uzalishaji wenye tija.
Kiongozi huyo,aliweza kufika nyumbani kwa Mzee Yangison Mtawa akiagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanamsaidia kutafuta soko la bidhaa anazozalisha mzee huyo baada ya kuambiwa kuwa amekuwa akisubiri tu matukio kama vile nane nane na kimondo baada ya hapo bidhaa alizozalisha kwa gharama zikihifadhiwa.
Safari hiyo ikiendelea kwa kuupanda mlima Kashima ambao kwa madereva wengine huwa ni kipimo tosha cha fani hiyo kutokana na kona kali zilizofunikwa na misitu ya asili inayoongeza radhaa a utalii.
Alipofika katika Mradi wa Shamba la Miti wa Iyondo Mswima aliweza kupokea taarifa ya mradi huo toka kwa Meneja wa Shamba Ndg.Deograsian Kavishe akiridhishwa na taarifa hiyo jinsi inavyoakisi uhalisia wa mazingira ya eneo hilo na kuwa kivutio tosha cha kitalii.
Msafara ulielekea shambani ilikopandwa miti,huku macho yakiendelea kufaidi mandhari nzuri ya vilele vya milima vilivyofunikwa nyasi fupi ambazo baadaye zaweza potea kutokana na kufunikwa na miti inayoendelea kupandwa.
Mara baada ya kufika sehemu maalum iliyokuwa imeandaliwa lilifanyika tukio la kukumbuka ya kuzaliwa kiongozi huyo ikifurahiwa na kila mmoja kutokana na mahali ilipoandaliwa huku ikinyunyiziwa na manyunyu yaliyoshuka polepole yakiashiria neema na utukufu wa Mwenyezi Mungu.
Mwisho wa safari yake ilikuwa ni katika Maporomoko ya Lusalala yaliyopo kwenye Mto Sange ambako kuliweza kuwatoa jasho watalii hao wa ndani kutokana na mteremko mkali ambao haukuonesha kumteteresha Brigedia Jenerali huyo mstaafu.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa