Mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 zazinduliwa mkoani Songwe
Mbozi-Songwe
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amezindua Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2019 akisisitiza ujumbe wa mwenge kutekelezwa kwa vitendo ili kuleta matokeo chanya ikiwemo kupunguza maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Alisema kuwa maambukizi ya VVU na UKIMWI kwa mikoa ya Njombe,Iringa na Songwe ni makubwa ikilinganishwa na maeneo mengine hapa nchini hivyo mbio za mwenge zizae matunda ya kushuka kwa kiwango cha maambukizi kwa mikoa hiyo na taifa kwa ujumla.
Akizungumza na watanzania kwenye viwanja hivyo vya Kimondo vilivyopo kati ya Mlowo na Vwawa wilayani Mbozi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa aliwapongeza wananchi wa Songwe,mikoa ya jirani na taifa kwa ujumla jinsi walivyokuwa wamejitokeza kwenye uzinduzi huo wakiweka kando itikadi za kisiasa na kutanguliza uzalendo kwenye masuala ya kitaifa.
Kupitia nyimbo,mashairi na sanaa vikundi mbalimbali viliweza kuelezea namna waasisi wa taifa hili hayati Mwl.J.k.Nyerere na Abeid Karume walivyoweza kujenga misingi imara ya utaifa ambayo haina budi kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
Kikundi cha J.K.T Mlale toka mkoani Ruvuma kwa nyimbo zake kilionesha jinsi jeshi hilo linavyowajenga vijana wa nchi nzima katika kutumia sanaa kuwaunganisha watanzania.
Mkoa wa Songwe ulio na umri mchanga kuliko mikoa yote hapa nchini umebahatika kupewa heshima ya kuzindua mbio hizo kwa mwaka huu hali inayoweza kuwa chachu ya kuutambulisha zaidi kitaifa na kimataifa.
Kilele cha mbio hizo kinatarajiwa kufanyika mkoani Lindi mnamo Oktoba ,14 mwaka huu ukiwa ni utaratibu wa kukumbuka tarehe aliyofariki Baba wa Taifa hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere ukiwa umekimbizwa kwenye mikoa 31 yenye halmashauri/wilaya 195.
Ujumbe wa mwaka huu ni ‘’Maji ni haki ya kila mtu,Tutunze vyanzo vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa’’ pamoja na jumbe zingine ambazo ni ‘’Pima,Jitambue,Ishi’’,Nipo Tayari Kutokomeza Maralia Wewe Je?’’,Kataa Rushwa,’’Jenga Tanzania’’ na’’Tujenge Maisha Yetu,Jamii Yetu na Uhuru Wetu Bila Dawa za Kulevya’’.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa