Mkuu wa Wilaya ya Chitipa kutoka nchini Malawi Mhe.MaCMillani Magomero ameongoza timu ya watalaam wa utekelezaji wa Mradi wa Bonde la Mto Songwe kutembelea Wilaya ya Ileje kwa lengo la kujifunza uhifadhi wa mazingira.
Ugeni huo umeshiriki kikao cha pamoja na timu kama hiyo kutoka Wilaya ya Ileje ikiongozwa na Mkuu Wa Wilaya ya Ileje Mhe.Farida Mgomi.
Akifungua kikao hicho cha siku moja kilichofanyika katika Ukumbi wa VIM uliopo Itumba Mhe.Mgomi alisema kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa pande zote mbili kwa vile kila upande unahitaji kujifunza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Chitipa alisema kuwa kufanyika kwa ziara hiyo ni mwendelezo wa kuimarisha mahusiano ya kindugu yaliyojengwa na vizazi vilivyotangulia hata kabla ya mipaka hiyo kuwekwa na wakoloni.
Licha ya kufanya kikao hicho pia ugeni huo ulitarajiwa kutembelea vijiji vya Bulanga,Malangali na Ilondo vilivyoanza kutekeleza baadhi ya miradi ya awali inayohusiana na Mradi wa Uhifadhi wa Bonde la Mto Songwe ambao ni mpaka wa Tanzania na Malawi.
Lengo kuu la Mradi huo ni kuthibiti kuhamahama kwa Mto huo hususani katika Wilaya ya Kyela Tanzania na Karonga Iliyopo Malawi.
Taarifa za kikao hicho zilieleza kuwa kwenye vijiji vitakavyotembelewa vya Kata ya Malangali kuna miradi ya kilimo parachichi pamoja na kahawa ambayo pia ipo katika vijiji vya Njebete 1,Njebete 2 na Njebete 3 upande wa Malawi.
Mradi wa Uhifadhi wa Bonde la Mto Songwe unahusisha Wilaya za Kyela,Mbozi Ileje,Momba na Mbeya Vijijini kwa Tanzania pamoja na wilaya za Chitipa na Karonga kwa upande wa Malawi.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa