Wakazi wa Kijiji cha Isongole Wilayani Ileje mkoani Songwe wamepongezwa kwa jinsi wanavyounga juhudi za serikali katika kujiletea maendeleo hususani kwenye ujenzi wa miundo mbinu ya shule.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ndg.Haji Mnasi alipotembelea shule za Msingi Isongole na Mkumbukwa akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na matundu ya vyoo baada ya serikali kumwaga mamilioni ya pesa kwaajili ya kazi hiyo.
Akiwa katika Shule ya Msingi Isongole Mnasi aliweza kujionea ujenzi unaozingatia maagizo ya serikali ambapo zaidi ya matundu 42 ya vyoo yanatarajiwa kujengwa yakiwa ni matokeo ya pesa zilizotolewa na serikali pamoja na nguvu za wananchi.
Akiwa katika shule ya Msingi Mkumbukwa alifurahishwa kuwakuta wananchi wakiwa eneo la kazi huku mafundi wakizingatia maelekezo ya serikali.
Akizungumza na wananchi hao aliwataka kutambua kuwa fedha zinazotolewa na serikali ya Awamu ya Tano hii hazina budi kusimamiwa vema ili kunufaisha kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Kissa Kyalamwene Mwalimu Mkuu wa shule alimweliza kiongozi wake kuwa wamefikia katika hatua hiyo ya ujenzi kwasababu ya mshikamano baina ya viongozi na wananchi kwa ujumla.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Isongole Bi Nelly Mfwango aliongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa vyoo na madarasa kutaongeza chachu ya ufundishaji na ujifunzaji kwa vile shule hiyo inakabiriwa na mlundikano wa wananfunzi.
Akizungumza na kituo hiki kwenye ziara hiyo Kaimu Afisa Elimu Msingi Mwl.Bashiri Msegeya amesema kuwa jumla ya shilingi 131,598,643.56 zimetolewa kwa shule hizo mbili kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
Ziara ya kiongozi huyo iliishia katika Hospitali ya Wilaya ambapo aliweza kukutana na uongozi hospitali hiyo,kukagua majengo na kutoa maagizo ya kukamilisha maeneo yanayowahusu ili wananchi waanze kupata huduma badala ya kuendelea kuyaangalia tu majengo yasiyotoa huduma
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa