Ileje FM ambayo ni redio ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imeanza rasmi kurusha masomo kwa shule za msingi kuanzia Darasa la IV-VII redioni ili kuwasaidia wanafunzi kuendelea kupata elimu katika kipindi hiki cha janga la virusi vya corona.
Afisa Elimu Msingi wa Wilaya Mwl Godwini Mukaruka alisema wameamua kutumia ya redio ya kijamii ya Ileje FM 105.3 (Sauti ya Jamii) itakachotumika kurusha vipindi vya masomo kwa wakati wote wa janga hili.
Kwa nini redio Ileje FM?
Mwl. Mukaruka alisema redio inasikika maeneo mengi ya Wilayani hapa, hivyo wanafunzi watapata elimu katika kipindi ambacho shule zimefungwa kwa sababu ya Corona.
Aliongeza kuwa ili kufanikisha zoezi hilo vipindi vitakuwa vikirushwa kuanzia saa 2.00-4.00 Asubuhi kwa masomo mawili na 11.00 jioni kwa masomo mengine mawili huku wakitumia walimu waliopo wilayani humo.
Taarifa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri hiyo kupitia Idara ya Elimu Msingi ilieleza kuwa masomo yaliyoanza kufundishwa ni pamoja na Kiingereza,Kiswahili Sayansi na Maarifa ya Jamii.
Aidha, Mwl. Micheal Legonda Afisa Taaluma Elimu Msingi amesema utaratibu huo utasaidia kutokana na mrejesho anaoupata kupitia simu za wanafunzi wanaofuatilia vipindi hivyo.
Serikali ilisitisha masomo kuanzia shule za msingi hadi Vyuo Vikuu tangu Machi 17 huku njia mbadala zikichukuliwa kuhakikisha watoto hawakai bila kazi ambapo miongoni mwa njia za kuwafikia wanafunzi ni pamoja na kurusha masomo kwa njia ya redio, kama wilaya ya ileje ilivyoanza kufanya.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa