Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Ileje Bi. Nuru Waziri Kindamba amepongeza juhudi za Shirika la Amref Health Africa - Tanzania pamoja na UNICEF kwa kutekeleza mradi wa Interpersonal Communication – Immunization (IPC-I) ambao umechangia kuongeza kwa kiasi kikubwa utolewaji wa chanjo kwa watoto katika halmashauri hii.
DED Kindamba ameyasema hayo alipokutana na timu ya wataalam kutoka Amref Tanzania pamoja na UNICEF waliofika ofisini kwake kumweleza mafaniko yaliyofikiwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Aidha DED Kindamba ametoa rai kwa wadau kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi, akisisitiza kuwa ni dhamira ya serikali kuhakikisha inafanya kazi na wadau wote wa maendeleo ili kusogeza huduma kwa wananchi wote.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Shirika la Amref Tanzania, Dkt. Serafina Mkuwa alitoa shukrani kwa wafadhili UNICEF na kupongeza ushirikiano ambao timu ya utekelezaji wa mradi imepata kutoka serikalini kuanzia ngazi ya wizara, mkoa hadi halmashauri.
Mbali na kutekelezwa katika Wilaya yetu mradi huo umetekelezwa pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe chini ya ufadhili wa UNICEF na kusaidia kuinua kiwango cha utolewaji wa chanjo kwa watoto wadogo.
Aidha, katika kipindi cha utekelezaji wake, mradi wa IPC-I umetoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wametumika kuzunguka katika maeneo yao ili kutoa elimu juu ya umuhimu wa kupeleka watoto kliniki na kupata chanjo zote zinazotakiwa.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa