Wakati ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ileje koani Songwe ukiendelea Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ndg.Haji Mnasi ametembelea eneo la ujenzi na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa kwenye ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa nje (OPD)
Akiwa ameongozana na baadhi ya watalaam wa Ofisi yake Mnasi aliweza kukagua jengo hilo ambalo awali lilianza kujengwa na mkandarasi kabla ya Chuo Kikuu cha MUST Mbeya kupewa kazi hiyo.
“Niwapongeze sana Must kwa kazi nzuri mnayoifanya katika jengo hili,naamini kukamilika kwake mtakuwa mmeandika historia katika wilaya hii” aliwasifia DED huyo mara baada ya kumaliza ukaguzi.
Aliongeza kuw, miradi kama hiyo inapojengwa kwa viwango vinavyotakiwa inafungua milango mingine ya upataji fedha toka serikalini kwa kuwa viongozi wa juu huamini kuwa fedha hizo huenda kuwapunguzia kero wananchi wanyonge ambao serikali ya awamu hii inawapigania.
Naye Mhandisi Dickson Chigundu toka MUST anayesimamia jengo hilo aliahidi kuwa watahakikisha jengo hilo linajengwa kwa viwango vinavyotakiwa hali itakayoongeza hadhi ya chuo chao ambacho huzalisha pia watalaam wa ujenzi.
Janet Makoye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo alimweleza kiongozi huyo kuwa huduma kwa baadhi ya majengo zinatarajiwa kuanza kutolewa mara vifaa vitakapowasili.
Mpaka sasa serikali imeshatoa zaidi ya Shilingi Bilioni 1 na milioni 800 kwaajili wa upanuzi wa Hospitali ya Wilaya na zaidi ya milioni 900 kwaajili ya Vituo vya Afya vya Ibaba na Lubanda ambapo kukamilika kwake kutawapunguzia wananchi kwenda wilaya zingine na nchi jirani ili kupata huduma za afya.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa