WATENDAJI WAPYA WA VIJIJI ILEJE WATAKIWA KUTOIAIBISHA SERIKALI
Daniel Mwambene,Ileje
Zaidi ya Maafisa Watendaji 43 na mpishi mmoja wametakiwa kuepuka na vitendo vyote vinavyoweza kuizalilisha serikali kwenye vituo vyao vya kazi watakavyopangiwa.
Hayo yalitolewa na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe wakati wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya 44 kati ya 47 nafasi za Maafisa Watendaji wa vijiji na mpishi mmoja waliotakiwa kuwepo.
Akifungua mafunzo hayo ,Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ndugu Haji Mnasi aliwataka kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuipa heshima serikali katika maeneo yao ya kazi ambako ndiko waliko wananchi.
‘’Mnakwenda kufanya kazi na wananchi ambao ni walemgwa wa mipango yote ya nchi hivyo kafanye kazi mkibeba sura ya serikali ya nchi hii kwa kuepukana na vitendo vyote vinavyoiaibisha serikali kwa wananchi wake”,aliwambia kiongozi huyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa ,vitendo vyote vya aibu vinapofanywa na mtumishi wa umma kwa wananchi huhesabiwa kama vile vinafanywa na serikali hivyo hawana budi kuepukwa.
Pamoja na mambo mengine,kiongozi huyo aliwataka viongozi hao wa vijiji kwenda kuhakikisha mapato ya serilkali hayapotei na hawawi chanzo cha kupotea kwa mapato hayo akiahidi kutumia kama kipimo cha utendaji wa kazi wao.
Naye,mmoja wa watendaji wa wa Kikosi cha Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)Ndugu Julius aliwataka waajiriwa hao kuepukana na vitendo vyote vinavyochochea rushwa ikiwa ni ushiriki wao katika kupiga vita hali hiyo ambayo huathiri utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ikumbukwe kuwa,hadi kufikia hatua hii safari ya waajiriwa hawa ilikuwa ndefu ambapo katika kuomba hizo nafasi 47 karibu maombi 3000 yalipokekewa na walioitwa kwenye usaili ni 946.
Hata hivyo,kati ya waajiriwa 46 wa nafasi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji waliofika ni 43 na mpishi huyo mmoja jumla yao wote ni 44 huku watatu wakiwa hawajafika kwenye hatua hii ya kujaza mikataba ya ajira
Ajira hizi zimekuja ikiwa ni hatua baada ya watendaji wa vijiji waliokuwepo kukosa sifa kulingana na mikataba yao ya ajira ya mwaka 2014 ambapo wale wa Darasa la Saba walitakiwa kujiendeleza hadi kufikia Elimu ya Kidato Cha nne.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa