Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yamefanyika mapema leo tarehe 6 Juni 2025 katika Wilaya ya Ileje, yakihudhuriwa na wauguzi kutoka vituo mbalimbali vya afya na zahanati. Maadhimisho hayo yaliongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Andrew Peter Mtui, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo. Katika hotuba yake, Mtui amewataka wauguzi kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa huku wakizingatia maadili, kanuni, na miiko ya taaluma yao ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi wanaopokea huduma.
Katika kuimarisha huduma kwenye vituo vya afya, Kaimu Mkurugenzi huyo amewataka wauguzi wafawidhi kuhakikisha wanasimamia vyema mapato kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa GOTHOMIS. Alisema kuwa usimamizi madhubuti wa mapato kupitia mfumo huo utaviwezesha vituo vya afya na zahanati kupata fedha zinazohitajika kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali, hivyo kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Aidha, Mtui ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa ajira katika sekta ya afya, hususan kwa wauguzi. Alisema kuwa ajira hizo si tu zinapunguza uhaba wa watumishi katika sekta hiyo muhimu, bali pia zinaboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kuchangia katika ustawi wa jamii. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wahudumu wa afya kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa