Katika kuwapunguzia gharama wananchi za kuwafuata viongozi wilayani ili kupeleka kero zao, viongozi wa wilaya ya Ileje mkoani Songwe wamejiwekea utaratibu wa kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kufanya mikutano ya hadhara.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wamepongeza utaratibu huo wa aina yake na kuoeleza kuwa suala hilo liwe ni endelevu kwakuwa limekuwa likijibu kero zao nyingi na kutatuliwa kwa wakati kupitia majibu ya papo kwa papo.
Mmoja wa wakazi wa Isongole Mchungaji Nikusubila Mwampashi, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Ndugu Haji Mnasi kwa kukutana na wananchi wake akiwa pamoja na Wakuu wa Idara ambao kwa pamoja waliweza kupokea maswali na kero zaidi ya 20 na kuzitolea ufumbuzi wa majibu wakati huo huo.
Alisema kuwa Mkurugenzi amefanya jambo muhimu hususani katika kupunguza kero za mara kwa mara zinazotokea katika kujenga mahusiano na mawasiliano mazuri baina ya wananchi na serikali yao kama Serikali ya Awamu hii inavyokwenda.
Katika mkutano mwingine kama huo kwenye kijiji cha Mbebe viongozi wa Halmashauri hiyo,waliweza kupokea kero mbalimbali ikiwemo bei ya mahindi ambapo kwa sasa debe linauzwa kati ya Tsh 3000/= hadi 4000/= ukizingatia kuwa mazao hayo yamezalishwa kwa gharama kubwa.
Wananchi hao pia waliomba Mradi wa TASAF wa kuhudumia Kaya maskini uweze kuwafikia wakazi wa kijiji hicho ambao awali waliukosa.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndugu Haji Mnasi aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza katika mikutano hiyo muhimu ambayo hueleza kero zao, akitoa maagizo kupitia haraiki hiyo alisema watendaji wake hawana budi kuhakikisha wanawafikia wananchi hao mpaka ngazi za vitongoji ambako ni msingi wa Serikali za Mitaa.
Aidha ikiwa ni moja kati ya mikutano yake Mkurugenzi pindi alipotembelea katika sekondari ya Ngulugulu, Mtendaji huyo aliwataka watumishi wa umma kutokuwa chanzo cha migogoro katika jamii ambayo imekuwa ikikwamisha maendeleo na kuchelewesha huduma kwa wananchi.
Na ikumbukwe kuwa ziara hizo zinatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine hasa yale ambayo hayajatembelewa na viongozi wa ngazi ya wilaya kwa muda mrefu ambapo kwanza huanza kwa kukutana na Serikali za Vijiji kisha hufanya mikutano ya hadhara.
Kadhalika kutokana na mshikamano uliopo baina ya serikali na wananchi, wilaya ya Ileje imekuwa moja ya wilaya zinazofanya vizuri katika ngazi ya mkoa na kitaifa kwa ujumla ambayo hutoa taswira nzuri kwa nchi jirani za Malawi na Zambia ambazo zimekuwa zikiingia kupitia mpaka huo wa nchi ya Tanzania.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa