Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Ileje imetembelea na kukagua Mradi wa Makaa ya Mawe Kiwira sambamba na vitalu vya makaa ya mawe katika eneo la Ileje lililopo mpakani na Wilaya ya Kyela.
Katika Kamati hiyo ambayo imeongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya yetu ambaye pia ni Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Bupigu Mhe. Ubatizo Songa imebaini uchimbwaji usiokuwa rasmi wa makaa ya mawe ambapo kwa kiasi kikubwa makaa hayo yamechimbwa katika eneo la Wilaya ya Ileje na kuuzwa katika eneo la Wilaya ya Kyela hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mapato yaliyotakiwa kuingia upande wa Ileje.
Katika ziara hiyo Kamati imebaini kuwa changamoto kubwa iliyopelekea wawekezaji hao kuuzia makaa ya mawe katika eneo la Kyela ni kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki katika eneo la upande wa Ileje hivyo kulazimisha muwekezaji kuuzia makaa hayo upande wa Kyela na hivyo kuchepusha mapato stahiki.
Aidha, pamoja na kubaini mapungufu hayo Kamati kupitia kwa Mwenyekiti wake ambaye ni Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mhe. Ubatizo Songa imedhimia kuondoka na mkakati wa kuhaklikisha makaa hayo yam awe hayatainufaisha tena Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ikiwa ni pamoja na kuandaa mazingira au miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwezesha ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo ili Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ianze kunufaika na rasilimali hiyo.
“Lakini kwa mkakati ambao tutakwenda nao tutakapokwenda kwenye majumuisho ni kuhakikisha haya makaa hayawanufaishi tena Kyela kwa maana kama makaa ya kwao tunaondoka na mkakati wa kuhakikisha tunaweka watu ambao watakuwa ni wakusanya ushuru katika eneo letu la Ileje kabla hayajafika kwenye eneo hili la Kyela.” amesema Mhe. Songa.
Katika hatua nyingine Kamati ilifanya ziara hadi eneo la Kiwanda cha Mradi wa Makaa ya Mawe Kiwira-Kabulo ambapo Kamati ilipokea taarifa kutoka kwa Mratibu wa Mradi Mhandisi Peter Maha ambapo mbali na kubaini changamoto kadhaa Kamati ilitoa maagizo na maelekezo kwa Uongozi wa kiwanda hicho kuongeza uzalishaji ili kuweza kukidhi mahitaji ya wateja.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa