TTCL kujenga kituo cha maunganisho cha mkongo wa Taifa wilayani Ileje ambapo mpango wake ni kuhakikisha Wilaya nzima ya Ileje pamoja na maeneo ya nchi jirani za Malawi na Zambia zinapata huduma ya uhakika ya mawasiliano kwa muda wote.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mhe. Farida Mgomi akiongea wakati wa kikao maalumu na Mkurugenzi wa TTCL katika Mikoa ya Songwe na Mbeya Mhandisi Mujuni kyaruzi ambaye ameambatana na wataalamu kutoka Makao Makuu amesisitiza juu ya umuhimu wa kutambua mchango wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwajali wananchi wa Ileje pamoja na nchi jirani kwani Serikali chini ya utawala wake imetoa zaidi ya Bilioni 45 kuhakikisha programu hii ya kusambaza mkongo wa taifa inatekelezwa na kuleta ufanisi kwa wananchi hususan kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya Sayansi na Teknolojia.
"Sote tumeshuhudia maboresho makubwa sana ya mkongo wa Taifa wa mawasiliano kimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 45 kwa ajili ya maboresho ya huo mkongo wa taifa wa mawasiliano." amesema DC Mgomi.
Aidha Mtaalamu kutoka TTCL Bw. Edson Richard amesema lengo Ileje kama Wilaya imepata nafasi ya upendeleo kwani itakuwa na njia mbili za mkongo wa taifa wa mawasiliano ambayo moja itatoka Tunduma hadi Ileje na nyingine itatoka Ileje hadi Kasumulu ambapo nchi jirani za Malawi na Zambia kwa pamoja zitanufaika na mradi huu.
Bw. Edson amethibitisha kuwa zoezi hili litakuwa ni la muda mfupi sana kwani linatarajia kukamilika mwezi Mei mwaka huu na hivyo kuhakikisha Wilaya nzima ya Ileje kutokuwa na tatizo la mtandao kabisa.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa