Katika kuimarisha ulinzi wa afya ya umma katika maeneo ya mipakani, siku ya leo Wilaya ya Ileje mkoani Songwe imeandaa kikao cha ujirani mwema kilichowakutanisha viongozi na wataalamu kutoka mataifa ya Tanzania, Malawi na Zambia kwa lengo la kujadili kwa pamoja mbinu za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayoathiri maeneo ya mpaka.
Kikao hicho kimehusisha wataalamu wa afya, wajumbe wa kamati za usalama kutoka wilaya zote za mipakani pamoja na maafisa waandamizi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, ambapo kwa pamoja walibadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuandaa mpango kazi wa pamoja kwa ajili ya kupambana na magonjwa kama vile kipindupindu, homa ya nyani na virusi vya Marburg.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Isoka nchini Zambia Mheshimiwa Jairus Simbeye alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu baina ya mataifa jirani ni njia pekee ya kuhakikisha kuwa magonjwa ya mlipuko yanatokomezwa kikamilifu. Kwa upande wa Malawi, Mkuu wa Wilaya ya Chitipa Mheshimiwa Gift Msowoya alieleza kuwa jitihada za utoaji elimu kwa jamii ni msingi mkubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko.
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Afisa Tawala Bwana Donbosco Komba alieleza kuwa mataifa hayo matatu yanapaswa kuendelea kubadilishana uzoefu, kuimarisha mawasiliano ya kikanda, pamoja na kuandaa mipango kazi ya pamoja yenye utekelezaji wa haraka.
Mbali na mijadala ya kimkakati, kikao hicho kiliambatana na semina mbalimbali zilizolenga kutoa mbinu bora za kuzuia na kukabili magonjwa ya mlipuko. Mafunzo hayo yalilenga pia kuhamasisha uandaaji wa mipango kazi inayoweka mbele afya ya jamii hususan katika maeneo ya mipakani.
Katika hitimisho la kikao hicho, wajumbe wote walikubaliana kuwa ni lazima elimu iendelee kutolewa kwa wananchi kwa njia endelevu ili kujenga uelewa wa namna bora ya kujikinga na magonjwa hatari. Kikao hicho kimebeba ujumbe mzito wa mshikamano, maarifa na hatua, na kinatarajiwa kuwa chachu ya ushirikiano wa muda mrefu wa kikanda katika kulinda afya za wananchi wa Tanzania, Malawi na Zambia
.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa