Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ileje imemaliza minong’ono iliyokuwepo miongoni mwa wananchi baada ya leo Januari, 29, 2023 kufikia maamuzi ya sauti moja kuwa ofisi za halmashauri zitajengwa hapo zilipo sasa na si vinginevyo.
Mjadala huo ulikuja ikiwa ni sehemu ya ajenda za kikao cha leo ikiwa imewasilishwa na menejimenti kwaajili ya kuchakatwa na kikao hicho ambacho ndicho cha juu katika kutoa maamuzi kwenye halmashauri za wilaya
Awali,Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ilitoa maelezo ya kuwa ilikuwa inapendekeza jengo la ofisi za halmashauri kujengwa katika Kitongoji cha Ipapa kilichopo Kijiji cha Isongole kwa lengo la kupanua mji na kuharakisha maendeleo pia ndilo lilitumika kuombea pesa hizo.
Ales Kaponda toka Idara ya Ardhi akisoma mapendekezo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji alisema kuwa mapendekezo hayo yalilenga eneo la kiwanja Na.203 Kitalu A-Isongole likiwa na ukubwa wa ekari 9.5 sawa na vigezo vya Mipango Miji pamoja na mahitaji ya ofisi za halmashauri ya wilaya.
Mhe.Samweli Kibona Diwani wa kata ya Kafule akiwa mchangiaji wa kwanza alipinga hoja hiyo huku akipigiwa makofi ya kuungwa mkono na Wahe.Madiwani alisema kuwa kuhamisha ofisi za halmashauri na kuzipeleka katika kijiji kingine kunaondoa kabisa maana halisi ya jina la Makao Makuu ya Wilaya yaani Itumba.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe,Ubatizo Songa akishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa lengo hilo alipigilia msumali wa mwisho kuwa eneo la sasa ndipo patakapojengwa ofisi hizo mpya baada ya serikali kutoa Tzsh.Bilioni Moja kwaajili ya ujenzi wa jengo la kisasa.
Nje ya kikao Mhe.Yotamu Ndile Diwani wa Kata ya Mlale pia amendelea kuishukuru serikali kwa mamilioni za miradi ya maendeleo akisema kuwa zinazidi kuisogeza mbele wilaya ya Ileje na akashukuru maamuzi ya busara yaliyofanywa na Wahe.Madiwani katika suala hilo.
Viongozi wa wilaya hiyo akiwemo Mhe. Mbunge alikuwa akionekana kukerwa na hali ya majengo hayo ya halmashauri ambayo ni ya pili kwa ukongwe katika Mkoa wa Songwe ikizidiwa na Mbozi.
Kila walipofanya ziara viongozi wa kitaifa akiwemo Mhe.Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliweza kuzungumzia juu ya kukosekana kwa ofisi za kisasa za halmashauri wakiahidi kufanyia kazi hali inayoonesha matunda ya ahadi zao.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa