Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe.Omary Mgumba wakati wa ziara yake ya siku moja alipotembelea migodi miwili ya Makaa ya Mawe ule wa Kaburo na Kiwira iliyopo wilayani Ileje Mkoani humo.
“Nawapa siku tatu TARURA Ileje watoe maelezo kwanini wamebadili matumizi ya fedha bilioni saba zilizotengwa na serikali na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwaajili ya ujenzi wa barabara inayotoka Kaburo-Mwalisi hadi STAMICO-Kiwira ‘‘alihoji Mhe. Mgumba”.
Mgumba ameongeza kuwa TARURA wameiondoa kwenye mpango wa kujenga barabara hiyo na fedha zake kuelekezwa kwenye barabara zingine wakitaka STAMICO wajenge wenyewe kutokana fedha za mapato yao ya ndani akisema kuwa TARURA kwa kufanya hivyo wamedharau maamuzi ya serikali na bunge.
Kiongozi huyo amesema kuwa bunge lilitenga Bilioni saba likitambua umuhimu wa barabara hiyo yenye urefu wa Km 7 ambayo ingerahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka Mgodi wa Kaburo hadi Mgodi wa Kiwira ambapo pana mtambo wa kuchakata rasilimali hiyo ambapo kwa sasa magari hulazimika kuzunguka umbali wa kilomita 38 kupitia Wilaya za Kyela na Rungwe.
“Barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Ileje, Songwe na taifa KWA kwa ujumla hivyo,itakapokamilika itasaidia kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe pamoja na kuongeza ajira‘‘alisema Mgumba”.
Mgumba amesema ujenzi wa barabara hiyo uzingatie mahitaji kwani magari yenye uzito wa tani 30 yatapita kwa ajili ya kubeba makaa yam awe.
Akizungumzia kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara(Tanganyika wakati huo) alisema kuwa Mgodi wa Kiwira ni moja ya alama za Baba wa Taifa alizotuachia Watanzania zikionesha ubunifu katika uongozi hivyo kuendelea na uzalishaji ni sehemu za kuwaenzi waasisi hao.
Samweli Kibarange Mratibu wa Shughuli za Makaa ya Mawe Kiwira amesema ujenzi wa barabara ya kilomita saba utakapokamilika utaongeza kasi ya uzalishaji na kuleta ushindani katika soko la dunia.
Aidha,Kibarange ameiomba serikali ihamasishe wamiliki wa viwanda vya saruji vya ndani na nje kununue makaa ya mawe kutoka STAMICO kwani uzalishaiji wake ni wa kuridhisha ambapo kwa mwaka ujao wanatarajia kuzalisha zaidi ya tani milioni moja na laki tano.
Diwani wa kata ya Ikinga ambako migodi hiyo ipo Mhe.Sadock Nyingi amepongeza juhudi za Mkuu wa Mkoa kwa kutembelea kata yake akisema ni ufunguzi wa ukurasa mpya katika kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa