Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe.Godfrey Kasekenya Msongwe ambaye ni Mbunge wa Ileje amewataka watumishi wa umma kutokuwa kikwazo katika kuimarisha Diplomasia ya Uchumi.
Kasekenya aliyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Isongole mara baada ya kupokea kero za wakazi wa eneo hilo waliomwomba kupunguziwa ushuru mkubwa wanapoingiza nchini mazao ya nafaka toka nchi jirani.
Alisema kuwa serikali imetumia fedha nyingi kujenga barabara ya lami kutoka Mpemba-Momba hadi Isongole-Ileje zaidi ya Km 50 na kuunganisha barabara hiyo na nchi jirani ya Malawi kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo ya zikiwemo biashara halali za mpakani.
Aliongeza kuwa,kuwaongezea ushuru wananchi kunapunguza kasi ya ukuaji wa Diplomasia ya Uchumi ambayo Taifa serikali inaona kuwa ni fursa ya kufungua masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Serikali haikukurupuka kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami,bali ni mipango mahsusi ya kuhakikisha biashara za mpakani zinafunguka”.Alifafanua kiongozi huyo ambaye kitaaluma ni Mhandisi.
Alisema kuwa serikali tayari imeshaanza kufanya upembuzi juu ya ujenzi wa barabara ya Isongole hadi Kyela kupitia Kata za Bupigu,Malangali,Kafule na Ikinga kwa Lengo hilo la kufungua milango ya biashara kitaifa na kimataifa.
Kwenye mkutano huo wa hadhara wananchi walimwomba kufikisha kilio chao kwenye wizara husika ili kurahisha upatikanaji wa Hati za Kusafiria nje ya nchi ambapo hulazimika kuzifuata hadi Vwawa Mkoani.
Wakazi wa Wilaya ya Ileje pamoja na wasafiri toka nchi jirani ya Malawi wamekuwa wakipongeza juu ya ujenzi wa barabara ya Mpemba hadi Isongole kwa kiwango cha lami ambayo wamekuwa wakitumia sana kwenda Tunduma kununua bidhaa za dukani huku nauli ikishuka kutoka 4,000/= hadi 2,000/=
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa