Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, ametoa wito kwa wakulima wa zao la pareto wilayani humo kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kukidhi mahitaji ya soko na kupata faida inayowawezesha kujikimu kimaisha. DC Mgomi alitoa rai hiyo mapema leo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya zao la pareto katika kata za Ibaba na Itale ambazo ndizo zinazolima zao hilo kwa wingi.
Katika ziara hiyo, DC Mgomi aliwahimiza wakulima kuimarisha ushirikiano baina yao kwa kushirikiana, kusaidiana na kuwahamasisha wakulima wengine kujiunga katika kilimo cha pareto. Alibainisha kuwa bado kuna ardhi ya kutosha inayoweza kutumika kuongeza wigo wa uzalishaji, hivyo ni muhimu kwa wakulima kutumia fursa hiyo kukuza uchumi wao na wa jamii kwa ujumla.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia ubora wa zao hilo ili bidhaa zinazokwenda sokoni ziwe katika viwango vinavyokubalika na hatimaye kuwanufaisha wakulima kwa kupata faida mara mbili. DC Mgomi alisema kuwa ubora wa pareto ndio msingi wa kupata bei nzuri sokoni na kuwaongezea wakulima motisha ya kuendelea na kilimo hicho kwa tija.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mgomi aliwatoa hofu wakulima hao kwa kuwahakikishia kuwa Serikali kupitia Bodi ya Pareto (COPRA) itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwapatia mbegu bora pamoja na kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika. Alisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja na sekta ya kilimo.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa