Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mheshimiwa Farida Mgomi, amewakaribisha rasmi madaktari bingwa katika hafla maalum iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kutoa huduma za afya za kibingwa kwa wananchi, chini ya mpango unaoendelezwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Mgomi aliwakaribisha madaktari hao kwa moyo wa upendo na mshikamano, huku akiwaahidi ushirikiano wa karibu kutoka kwa uongozi wa wilaya pamoja na jamii nzima ya Ileje. Aidha, alitoa pongezi na shukrani kwa Rais kwa kuendeleza juhudi za kuboresha ustawi wa afya ya Watanzania kupitia kampeni hii ya Madaktari Bingwa.
Madaktari bingwa hao wanatarajiwa kutoa huduma mbalimbali za matibabu ya kibingwa kuanzia tarehe 26 hadi 31 Mei katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje, ambapo wananchi watahudumiwa kwa huduma za kitaalamu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Wananchi wote wa Ileje na maeneo ya jirani wamehimizwa kujitokeza kwa wingi katika kipindi hicho ili kunufaika na huduma hizo muhimu, ambazo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha huduma za afya nchini.
Haki Miliki Haki Zote Zimehifadhiwa